Umoja wa Mataifa wapiga kura kutaka usitishaji mapigano Gaza
13 Juni 2025
Azimio hilo limetaka pia kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas, na kufikishwa haraka misaada kwa takribani Wapalestina milioni mbili wenye mahitaji makubwa ya chakula kwenye Ukanda huo.
Mataifa 149 wanachama wa Umoja huo yalipiga kura kupitisha azimio hilo dhidi ya 12 yaliyokataa na 19 yaliyojizuwia kupiga kura zao kwenye Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa hapo jana.
Soma zaidi: Kura nyingine ya Baraza la Usalama la UN kuhusu Gaza
Marekani na mshirika wake wa karibu, Israel, sambamba na Argentina, Paraguay, Papua New Guinea na mataifa sita ya visiwa vya Pasifiki ndiyo yaliyopiga kura kupinga azimio hilo.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, amesema operesheni za misaada huenda zikashindwa kabisa kwenye Ukanda huo baada ya Israel kuukatia mawasiliano yote ya simu. Haya yanajiri wakati mashambulizi ya kijeshi ya Israel yakiendelea kote Gaza.