Umoja wa Mataifa wapitisha azimio la kumlaani Assad
16 Mei 2013Wakati maneno yake hayana nguvu ya kisheria, maazimio ya baraza hilo lenye wanachama 193 yanaweza kubeba uzito mkubwa wa kimaadili na kisiasa. Mataifa 107 yalipiga kura ya ndiyo dhidi ya 12 za hapana, wakati mataifa 59 yalijizuia. Hii iliwakilisha kushuka kwa kiwango cha uungwaji mkono ikilinganishwa na azimio la kuilaani serikali ya Syria lililopitishwa mwezi Agosti mwaka jana kwa kura 133 za ndiyo, dhidi ya 12 za hapana na 31 waliojizuia.
Sababu za kushuka kwa uungwaji mkono
Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa waliezea wasiwasi kuwa huenda Syria iko katika mchakato wa kubadilisha utawala, unaoongozwa na serikali za kigeni, na hofu juu ya kuimarika kwa makundi yenye msimamo mkali miongoni mwa waasi, kama sababu za kupungua kwa uungwaji mkono wa azimio hilo. Urusi, ambayo ni mshirika wa karibu zaidi wa utawal mjini Damascus, ilipinga vikali azimio hili lililoandaliwa na Qatar, ambayo serikali ya Assad inaishtumu kwa kuwapatia silaha waasi.
Wanadiplomasia wamesema ujumbe wa Urusi uliwaandikia barua wanachama wote wa Umoja wa Mataifa ukiwasihi kupinga azimio hilo ambalo ulisema linadhoofisha juhudi za Marekani na Urusi kuandaa mkutano wa amani ambao utajumuisha pia serikali ya Assad ma waasi, ambao waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry, anasema unaweza kufanyika mapema mwezi Juni.
Marekani yatetea
Lakini naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Rose DiCarlo alisema azimio hilo halipingani na mpango wa Marekani na Urusi. "Kwa mtazamo wetu, azimio lililoko mbele yenu linaambatana na mpango wa hivi karibuni. Kupitishwa kwa azimio hili kutatuma ujumbe kwamba suluhisho la kisiasa tunalolitafuta sote ndiyo njia bora ya kumaliza mateso ya watu wa Syria."
Azimio hilo linailaani serikali ya Bashar al-Assad kwa mambo makuu mawili: Ongezeko la matumizi ya silaha nzito katika maeneo ya raia, na kile muandaji wa azimio hilo, Qatar, ilichokiita utaratibu wa ukiukaji wa haki za binaadamu. Pia linaelezea wasiwasi kuwa utawala wa Assad unatumia silaha za kemikali, linatoa wito wa kuruhusiwa kwa wachunguzi wa Umoja wa Mataifa ndani ya Syria, na kuundwa kwa serikali ya mpito inayoongozwa na Wasyria wenyewe, ikiwa na Muungano wa Taifa kama mwakilishi halali wa raia wa Syria.
Waliouawa wakaribia laki moja
Azimio hilo limepitishwa baada ya tangazo lililotolewa na Vuk Jeremic, rais wa baraza la Umoja wa Mataifa, kuwa idadi ya vifo vilivyotokana na mgogoro huo imefikia si chini ya 80,000, wakati shirika lauangalizi wa haki za binaadamu nchini humo likisema watu wasiopungua 94,000 wameuawa, na kwamba idadi hiyo inaweza kufikoa 120,000.
Nchini Syria kwenyewe, shirika hilo liliripoti kuwa vikosi vya serikali vikisaidiwa na vifaru na ndege za kivita, vilizuia shambulio dhidi ya gereza katikati mwa Aleppo, baada ya waasi kuripua ukuta wa gereza hilo ambalo lina wafungwa 4,000. Na mjini Damascus, mripuko mkubwa ulitikisa uwanja wa Umayyad, huku makabiliano yakiripotiwa katika mkoa wa kati wa Hama.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,afpe,ap
Mhariri: Mohammed Khelef