1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa: Dola bilioni 5 zahitajika kwa Afghanistan

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
12 Januari 2022

Umoja wa mataifa unatafuta dola bilioni 5 kwa ajili ya kuwasaidia mamilioni ya Waafghanistan wakati ambapo nchi hiyo inakumbwa na mgogoro wa kibinadamu na uchumi.

Afghanistan | Welternährungsprogramm der UN in Kandahar
Picha: Sanaullah Seiam/Xinhua/picture alliance

Umoja wa Mataifa umesema unahitaji kiasi hicho cha dola bilioni 5 kwa mwaka 2022 ili kukabiliana na janga la kibinadamu nchini Afghanistan na pia msaada huo utatumika kurejesha uthabiti kwenye taifa hilo linaloandamwa na misukosuko kwa zaidi ya miaka 40.

Mwito huo ulizinduliwa hapo jana Jumanne na Umoja wa Mataifa umesema kiwango hicho cha fedha ambacho ni kikubwa zaidi kuwahi kuombwa kulisaidia taifa moja, kitawasaidia raia wa Afghanistan wapatao milioni 22 wakiwemo raia wa Afghanistan milioni 5.7 ambao ni wakimbizi walioko nje ya nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa umeelezea kwamba dola bilioni 4.4 zinahitajika kutumika ndani ya Afghanistan na dola milioni 623 zitatumika kuwasaidia mamilioni ya waafghani walioikimbia nchi hiyo.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin GriffithsPicha: Denis Balibouse/Reuters

Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths, aliyeanzisha kampeni hiyo amesema mgogoro kamili wa kibinadamu unakaribia na kwamba ni ipo dharura ya kuzuia njaa, magonjwa, utapiamlo na vifo kwa watu wa Afghanistan.

Umoja wa Mataifa umesema mwito huo utasisitizwa kwenye mkutano wa utakaojadili ahadi za wafadhili utakaofanyika katikati ya mwezi Machi. Mataifa kadhaa yametangaza ufadhili wao mpya, unaojumuisha nyongeza ya dola milioni 308 kutoka Marekani na dola laki 5 kutoka Israel, na kuna dalili kwamba fedha zaidi zitapatikana kutoka mataifa mengine hasa ya Magharibi.

Tangu kundi la Taliban lilipochukua udhibiti wa nchi hiyo mwezi Agosti mwaka jana, Afghanistan imetumbukia kwenye mzozo mkubwa wa kifedha, mfumuko wa bei na ukosefu wa kiwango cha juu cha nafasi za kazi.

Chanzo:AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW