1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawimbi ya joto kali kuongezeka hadi miaka ya 2060-UN

Daniel Gakuba
20 Julai 2022

Umoja wa Mataifa umesema mawimbi ya joto kali kama yanayoikumba Ulaya Magharibi hivi sasa yatazidi kujitokeza mara kwa mara hadi angalau mwaka 2060, na kuongeza kuwa hili lapaswa kuwa onyo kwa wachafuzi wa mazingira.

Hitzewelle in Spanien
Picha: Ricardo Rubio/EUROPA PRESS/dpa/picture alliance

Mkuu wa kitengo cha utabiri wa hali ya hewa cha Umoja wa Mataifa  Petteri Taalas ameuambia mkutano wa wanahabari mjini Geneva, kuwa juhudi za binadamu za kupambana na mabadiliko ya tabianchi hazitasaidia pakubwa kuizuia hali inayoshuhudiwa sasa, lakini zinaweza kurekebisha mwelekeo wa matukio hayo baada ya miongo kadhaa kuanzia sasa.

Soma zaidi: Moto wa msituni wazusha sokomoko kusini mwa Ulaya 

Tangu wiki iliyopita, maeneo makubwa ya Ulaya kusini na magharibi yameshuhudia viwango vya joto vya kuvunja rekodi, ambavyo kwa mara ya kwanza vimevuka nyuzi 40 za Celsius nchini Uingereza. 

Nchi nyingi za Ulaya kusini na magharibi zimekabiliwa na joto la kuvunja rekodiPicha: Vuk Valcic/Zuma/picture alliance

Kilimo kuathiriwa vibaya na matukio haya

Taalas ameonya kuwa hali hii itakuwa na athari mbaya kwa kilimo miongoni mwa sekta nyingine.

''Tunatarajia kuona madhara makubwa kwa kilimo. Mawimbi ya joto yaliyoikumba Ulaya siku za nyuma yalisababisha hasara kubwa ya mavuno, na hali hii ya sasa inajiri tukiwa na mzozo wa chakula duniani kutokana na vita vya Ukraine,'' amesema Taalas. 

Afisa huyo amesema yumkini majanga yatokanayo na kuongezeka kwa joto duniani yatakuwa mabaya zaidi,  kwa sababu bado utoaji wa hewa chafu unazidi kuongezeka badala ya kupungua, hususan miongoni mwa mataifa makubwa kiuchumi barani Asia.

Ukame unaotokana na mabadiliko ya tabianchi umeathiri sana sekta ya kilimoPicha: Mauro Ujetto/NurPhoto/picture alliance

Afya ya wanadamu haitaepuka madhara ya mabadiliko haya 

Mkutano huo na waandishi wa habari ulilishirikisha pia Shirika la Afya Duniani, WHO, na afisa wake anayeshughulikia athari za kimazingira, Maria Neira amesema viwango vya juu vya joto vitatatiza namna mwili wa binadamu unavyojipanga kuratibu joto ndani ya viungo vyake, na hilo linaweza kusababisha mkururo wa magonjwa.

Neira amesema wimbi la joto lililoisibu Ulaya mwaka 2003 lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 70,000.

Uchafuzi wa hewa waongezeka badala ya kupungua

Huku hayo yakiarifiwa, wanasayansi na wataalamu wanaofuatilia utekelezaji wa hatua za mataifa za kutunza mazingira, wamesema kati ya pande zinazotoa kwa wingi hewa ya ukaa duniani, Umoja wa Ulaya pekee ndio ulioidhinisha sera zinazoendana na malengo ya dunia ya kudhibiti ongezeko la joto duniani.

Soma zaidi: UN: Afrika kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi

Wataalamu hao hata hivyo wameelezea wasiwasi kuwa Ulaya ambayo hivi sasa inakabiliwa na kizungumkuti kuhusu vyanzo vya nishati wakati wa msimu ujao wa baridi, huenda itageukia vyanzo vichafu vya kukidhi mahitaji ya watu wake, na hatua hiyo inaweza kuzishawishi nchi nyingine kufuata mfano huo.

-afpe,ape

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW