Yemen huenda ikakabiliwa na janga kubwa la njaa
9 Novemba 2017Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya kulitaarifu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa kikao cha ndani kuzungumzia juu ya mgogoro wa Yemen ambako majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia yamekuwa yakiendesha operesheni dhidi ya waasi wa kihuthi tangu mwaka 2015.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeyataka majeshi hayo ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kuliacha eneo la usafiri wa anga nchini Yemen huru pamoja na kufungua bara bara na bandari zilizofungwa ili kuruhusu usambazaji wa misaada ya kiutu katika taifa hilo ambalo kiasi ya watu milioni saba hivi sasa wanakabiliwa na njaa.
Balozi wa Italia katika Umoja wa Mataifa Sebastiano Cardi ambaye kwa sasa ndiye anashikilia urais wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa nchi wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wameonesha wasiwasi wao kuhusiana na hali mbaya inayoikabili kwa sasa Yemen na kusisitiza juu ya haja ya kuhakikisha kuwa njia kuu zote za usafiri nchini humo zinatumika kama kawaida.
Majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia yalifunga mipaka ya Yemen kufuatia shambulizi lililofanywa na waasi wa kihuthi ambalo lilizuiwa na majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia jirani na uwanja wa ndege wa mjini Riyadhi.
Umoja wa Mataifa ambao tayari umeitaja Yemen kuwa nchi inayoongoza duniani kwa kukabiliwa na mgogoro wa kibinadamu umeonya kuwa hali nchini Yeman kwa sasa ni mbaya.
Umoja wa Mataifa waitaka Saudi Arabia kufungua haraka njia kuu za usafiri
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizungumza kwa simu na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir jana Jumatano na kusema kulikuwa na dalili za uwezekano na kufunguliwa njia za usafiri wa kuingia nchini Yemen.
Kiasi ya watu milioni 17 nchini Yemen wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu umesababisha vifo vya watu zaidi ya 2,000 hadi sasa.
Hapo jana shehena ya shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu ya dawa zinazotumika kuzuia maradhi ya kipindupindu ilizuiwa mpakani kaskazini mwa Yemen.
Mkuu wa huduma za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa usafiri wa anga lazima urejeshwe haraka katika mji unaodhibitiwa na waasi wa Sanaa na mji unaodhibitiwa na serikali ya nchi hiyo wa Aden.
Hayo yanajiri wakati mamia kadhaa ya magari yakipanga msitari katika barabara kuu za mji mkuu wa Yemen baada ya waasi wanaodhibiti mji huo kuamuru hapo jana vituo vya mafuta vifungwe wakiwatuhumu wafanyabiashara wanaomiliki makampuni ya mafuta nchini humo kupandisha bei ya bidhaa hiyo kwa kisingizio cha hatua iliyochukuliwa na majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kufunga njia kuu za usafiri.
Bei ya mafuta imepanda kwa silimia 50 tangu Jumatatu wiki hii, ambapo msemaji wa wizara ya mafuta ya waasi wa kihouthi Hassan al-Zaydi amesema wafanyabiashara wa mafuta nchini humo wamekataa kutekeleza amri ya kurejesha bei ya mafuta kama kawaida hali iliyopelekea waasi hao kuamuru kufungwa vituo hivyo vya mafuta.
Mwandishi: Isaac Gamba/ APE/AFPE
Mhariri :Gakuba, Daniel