Umoja wa mataifa watahadharisha dhidi ya kuwabughudhi wakimbizi wa Somalia.
23 Julai 2010Umoja wa mataifa umesema leo kuwa wakimbizi kutoka Somalia wanabugudhiwa na kukamatwa nchini Kenya pamoja na jimbo lililojitangazia uhuru la Somalia la Puntland kutokana na shambulio la bomu lililofanywa na kundi la Waislamu wenye msimamo mkali la al-Shabaab nchini Uganda. hayo ameyasema msemaji wa shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, Melissa Fleming mjini Geneva.
Maafisa katika jimbo la Puntland wamewarejesha katika maeneo ya mzozo katikati ya Somalia wiki hii zaidi ya Wasomali 900 ambao wamekimbia makaazi yao, lakini hadi sasa Kenya haijawarejesha Wasomali ambao wanaweza kuthibitisha kuwa wana hadhi ya ukimbizi, amesema kamishna wa shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi.
Kutokana na mashambulio ya kigaidi hivi karibuni, tumegundua matukio kadha ya kibaguzi dhidi ya wageni, kukamatwa na kurejeshwa makwao Wasomali ambao wamekimbia mapigano, Melissa Fleming, msemaji wa wa UNHCR, amewaambia waandishi habari mjini Geneva.
Tunatoa wito kwa maafisa wa jimbo la Puntland kusitisha hatua hizi za kuwarejesha wakimbizi, ameongeza.
Watu wanaokimbia mapigano kusini na kati ya Somalia wanahitaji ulinzi wa kimataifa na kulazimishwa kurejea katika maeneo hayo kunaweka maisha yao katika hali ya hatari kubwa, kwa mujibu wa msemaji huyo wa umoja wa mataifa. Tunahofia kuwa wale ambao wamekimbia wakiwa na sababu muhimu , vijana katika umri wa miaka kati ya 18 na 25, mara nyingi wanalengwa katika kuingizwa katika makundi ya wapiganaji kama al-Shabaab, Fleming amesema.
Al Shabaab , kundi la waasi wa Kiislamu lenye msimamo mkali wa kidini likiwa na uhusiano na kundi la al Qaeda, linadhibiti sehemu kubwa ya kusini mwa Somalia , inayopakana na kaskazini mashariki ya Kenya, na linapigana kutaka kuiangusha serikali inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi katika taifa hilo lililoko katika pembe ya Afrika.
Wapiganaji wa Kiislamu nchini Somalia wamewauwa wanajeshi wawili wa jeshi la kulinda amani la Afrika , katika mji mkuu Mogadishu, amesema msemaji wa ujumbe wa umoja wa Afrika wa kulinda amani leo Ijumaa.
Wakati huo huo wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imetoa tamko la tahadhari ya kusafiri jana Alhamis kwa raia wa Marekani wanaotaka kwenda Kenya, ikielezea kuhusu kuongezeka kwa kitisho kutokana na shambulio la bomu la kujitoa muhanga mapema mwezi huu katika nchi jirani ya Uganda.
Ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi umewataka raia wa Marekani kuchukua tahadhari wawapo katika maeneo ya watu wengi na kuwaonya kuepuka kufika katika mikutano ya hadhara na maandamano.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani pia imeonya kuhusu uwezekano wa kutokea ghasia wakati wa kukaribia kura ya maoni kuhusu katiba mpya nchini Kenya.
Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE
Mhariri :