1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WMO yatahadharisha kuhusu kasi ya mabadiliko ya tabianchi

11 Novemba 2024

Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limetahadharisha tena kuhusu kiwango cha juu zaidi cha hatari wakati ambapo kuna kasi ya juu ya mabadiliko ya tabianchi ndani ya kizazi kimoja.

Katibu mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Celeste Saulo wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi mnamo Jumanne, Machi 19,2024
Katibu mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Celeste SauloPicha: MARTIAL TREZZINI/picture alliance

Ripoti hiyo ya WMO imesema kuwa wastani wa kiwango cha joto duniani ulikuwa wa kuvunja rekodi kwa nyuzi joto 1.54 juu ya kiwango cha kabla ya viwanda kati ya 1850 na 1900 na kuongeza kuwa watafiti wa WMO hawana imani kutakuwa na mabadiliko makubwa ifikapo mwisho wa mwaka.

Makubaliano ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Paris ya mwa 2015 yaliweka lengo la kupunguza ongezeko la joto kwa kiwango cha wastani cha muda mrefu kufikia nyuzi joto 1.5. Kulingana na WMO, ongezeko hilo kwasasa ni nyuzi joto1.3 kwa kuzingatia kiwango hicho.

WMO yasema haitapunguza malengo ya kiwango cha nyuzi joto 1.5

Katibu mkuu wa WMO Celeste Saulo, amesema kila kiwango cha ongezeko la joto ni muhimu na kwamba hawataondoa kiwango hicho cha nyuzi joto 1.5.

Saulo ameongeza kuwa kiwango cha mvua na mafuriko yaliyovunja rekodi, vimbunga vya kitropiki vinavyoongezeka kwa kasi,jotokali, ukame wa mara kwa mara pamoja na mioto mikali ya nyika ambayo imeshuhudiwa katika sehemu mbalimbali za dunia mwaka huu, kwa bahati mbaya ndio hali halisi ya sasa na picha ya mustakabali wa baadaye.

Nembo ya COP29 mjini Baku, Azerbaijan, Picha: Jakub Porzycki/NurPhoto/picture alliance

Katika makala iliyochapishwa kwenye gezeti la kila siku la Uingerezea la Guradian hii leo, mwanaharakati wa hali ya hewa Greta Thunberg ameushtumu mkutano huo wa COP29 na kuutaja kuwa ''utani mbaya.''

Thurnberg aitaja COP29 kama mkutano wa kutoa taarifa za uongo

Kwenye makala hiyo kwa jina, COP ya amani? Je ni vipi mamlaka ya Azerbaijan inayokiuka haki za binadamu inaweza kuwa mwenyeji? mwanaharakati huyo wa umri wa miaka 21, ameutaja mkutano huo kama ''kitendo cha kutoa taarifa za uwongo au za kupotosha kuhusu manufaa ya kimazingira ya bidhaa au shughuli .''

Mkutano wa kilele wa mazingira COP29 waanza Azerbaijan

Thunberg pia alibainisha kuwa uchumi mzima wa Azerbaijan ulijengwa kwa nishati ya visukuku, ambayo ilichangia takriban asilimia 90 ya mauzo ya nje ya nchi. Mwanaharakati huo pia amesema licha ya kile ambacho taifa hilo linaweza kudai, halina nia ya kuchukuwa hatua za hali ya hewa.

Thunberg ameongeza kuwa nchi hiyo ilikuwa inapanga kuongeza uzalishaji wa nishati ya visukuku na kwamba hatua hiyo haiendani kabisa na kiwango cha nyuzi joto 1.5 cha mkataba wa Paris wa hali ya hewa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW