1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu mgogoro wa wakimbizi Sudan

2 Mei 2023

Mapigano Sudan yameendelea katika mji mkuu Khartoum na mji jirani wa Omdurman licha ya pande mbili zinazohasimiana kutangaza zimeongeza muda wa kusitisha mapigano kwa saa 72.

Sudan | Kämpfe in Khartum
Picha: AFP/Getty Images

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba watu zaidi ya 800,000 huenda wameyakimbia mapigano na hali ngumu Sudan, ambako milipuko imeutikisa mji mkuu Khartoum kinyume kabisa na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosainiwa na majenerali wanaopigana. Machafuko hayo ya umwagaji ambao sasa yameingia wiki ya tatu, tayari yamesababisha wimbi kubwa la maelfu kwa maelfu ya raia wa Sudankukimbilia nchi jirani ikiwemo Misri, Chad na Jamhuri ya Kati.

Shirika linalowahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema linajiandaa kwa uwezekano kwamba watu 800,000 huenda wamekimbia mapigano Sudan. Mkuu wa shirika la UNHCR Filippo Grandi amesema katika taarifa yake kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twita kwamba ikiwa mapigano hayatakoma basi watu zaidi huenda wakaikimbia Sudan na kusababisha mgogoro wa wakimbizi.

Mkuu wa shirika la UNHCR Filippo GrandiPicha: DW

Hapo jana meli inayoendeshwa na Marekani iliwasili nchini Saudi Arabia ikitokea Sudan ikiwa imewabeba raia zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali. Meli nyingine inayomilikiwa na Saudia Abia pia ilitia nanga mjini Jeddah ikiwa na raia kutoka Sudan, kuongezea raia wengine zaidi ya 5,400 ambao ufalme huo umeshawapokea.

Wakati huo huo, Uingereza imesema inatafakari njia za kupeleka msaada wa kibinadamu Sudan kwa ushirikiano na washirika wake wa kimataifa, Umoja wa Mataifa na asasi zisizo za kiserikali, baada ya idadi kubwa ya raia wake kuondolewa kutoka nchi hiyo inayokabiliwa na machafuko. Serikali ya Uingereza imesema katika taarifa yake kwamba jumla ya watu 2,197 wamesarifishwa kutoka Sudan na kwamba imeunda timu katika mji wa bandari wa Port Sudan itakayotoa huduma za uhamiaji kwa raiaw a Uingereza, wakiwemo wale wanaoondoka kwa usafiri wa vyombo vya kibiashara.

Juhudi za upatanisho zashika kasi

Saudi Arabia ni miongoni mwa dola zenye nguvu katika eneo hilo zinazojaribu kuyafikisha mwisho machafuko ya Sudan. Mjumbe wa jenerali wa jeshi la Sudan Abdel Fattah Burhan, Dufallah al Haj Ali alikutana siku ya Jumapili mjini Riyadh na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan na anatarajiwa kuzuru Cairo kwa mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Misri leo Jumanne. Katika mkutano wa jumuiya ya nchi za kiarabu mjini Cairo jana Jumatatu, Misri ilipendekeza rasimu ya azimio linalotaka usitishwaji wa haraka wa mapigano.

Pande zinazopigana Sudan zimekubaliana kuwatuma wajumbe katika mazungumzo ambayo huenda yakafanyika nchini Saudi Arabia. Mjumbe maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa tume ya umoja huo nchini Sudan Volker Perthes amesema mazungumzo hayo yatalenga kutafuta makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyo imara na ya kutegemewa. Perthes aidha amesema jitihada za kuyashawishi majeshi rasmi ya serikali SAF na kikosi maalum cha wanamgambo RSF zimekumbwa na vizingiti.

Volker Perthes, Mjumbe maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa tume ya umoja huo SudanPicha: ASHRAF SHAZLY/AFP/Getty Images

Chama cha madaktari nchini Sudan kimesema katika taarifa kwamba kufikia jana Jumatatu raia 436 wameuwawa na wengine 2,174 wamejeruhiwa tangu machafuko yalipozuka Aprili 15.

Mkurugenzi wa Shirika la afya duniani WHO ukanda wa Mediterania mashariki Ahmed al-Mandhari ametahadharisha kwamba mapigano yanaishinikiza sekta ya afya ya Sudan na kuielekeza katika janga. Ametahadharisha juu ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, malaria na maonjwa mengine. WHO imetangaza makontena sita ya dawa yamewasili Port Sudan, mkiwemo vifaa vya matibau kwa ajili ya watu waliopata majeraha mabaya na wanaokabiliwa na utapiamlo mkubwa. Shirika hilo limesema mafuta ambayo ni haba wakati huu wa vita, yamesambazwa kwa hospitali kadhaa zinazotegemea majenereta.

Shirika la Mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFPlimesema linataraji hivi karibuni kuanza tena kusambaza chakula katika baadhi ya maeneo ya Sudan baada ya kusitisha shughuli zake kufuatia vifo vya wafanyakazi wake watatu wa kutoa misaada.

(afp,reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW