Umoja wa Mataifa wataka haki itendeke watoto waliouawa Iran
27 Machi 2026
Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amesema kushambuliwa kwa Skuli ya Msingi ya Shajareh Tayyebeh huko Minab nchini Iran kulibainisha "ukatili usioelezeka" dhidi ya watoto, na kwamba lazima kuwe na uwajibikaji kwa waliohusika.
"Dhima iko kwa wale waliofanya mashambulizi hayo kuchunguza kwa haraka, kwa usahihi, kwa uwazi na kwa kina. Maafisa wa ngazi za juu wa Marekani wamesema mashambulizi hayo yanachunguzwa. Ninatoa wito kazi hiyo ikamilike haraka iwezekanavyo, na matokeo yake yatangazwe hadharani. Lazima haki itendeke kwa madhara haya mabaya yaliyofanywa." Alisema Turk wakati akizungumza kwenye kikao cha Kamisheni yake mjini Geneva, Uswisi, siku ya Ijumaa (Machi 27).
Mkuu huyo wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa tafauti zozote ambazo mataifa yanaweza kuwa nazo haziwezi kutatuliwa kuwashambulia na "kuwauwa watoto wa skuli."
Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa awali yaliyochapishwa na jarida la New York Times, kombora la Marekani aina ya Tomahawk ndilo lililoipiga skuli hiyo kimakosa mnamo tarehe 28 Februari, lakini Marekani yenyewe haijawahi kukiri moja kwa moja kubeba dhamana ya mauaji hayo, huku Waziri wa Vita, Pete Hegseth, akiashiria kuwa mashambulizi hayo yalifanywa na Iran yenyewe.
Rubio kukutana na wenzake wa G7
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, aliwasili nchini Ufaransa siku ya Ijumaa kwa ajili ya mkutano na wenzake wa kundi la mataifa saba yenye nguvu kubwa kiuchumi ulimwenguni (G7) kujaribu kuwashawishi kukubaliana na vita vya Marekani dhidi ya Iran.
Ziara ya Rubio inafanyika siku moja tu baada ya Rais Donald Trump kuushambulia muungano wa kijeshi wa NATO kwa kusita kwake ama kukataa kujiunga na vita vyake dhidi ya Iran.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha baraza lake la mawaziri siku ya Alkhamis (Machi 26) mjini Washington, Trump aliuita muungano huo wa kijeshi kuwa "hauna lolote unalofanya."
"Sisi ndio tupo kwa ajili yao NATO, lakini wao hawapo kwa ajili yetu. Je, tunawahitaji? Hapana. Sikuwahi kufikiria kuwa tunawahitaji. Nilikuwa nawajaribu tu. Nilisema, ningelipenda kuwaona mukijitokeza. Leteni mashua zenu. Munaweza kupita kwenye Mlango Bahari wa Hormuz, na munaweza kuwalinda watu wanaorushiwa risasi. Lakini hawakufanya. Na hilo ni jambo dogo sana tu." Alisema Trump.
Hilo lilitazamiwa kuzidi kumpa Rubio kibarua kigumu cha kuwashawishi wenzake hao juu ya mkakati wa Marekani kuutatuwa mgogoro uliopo, ambao kimsingi unapingwa na mataifa yote yaliyosalia.
Lakini hata wata wakati anaondoka Washington hapo jana, Rubio alisema anajuwa kazi kubwa aliyonayo, lakini akasisitiza hakuwa anakwenda Paris kuwafurahisha mawaziri hao wa G7, bali kuitumikia nchi yake.
Miongoni mwa mataifa saba ya kundi hilo, ni Japan pekee ambayo si mwanachama wa muugano wa kijeshi wa NATO.
Yaliyosalia - Marekani yenyewe, Uingereza, Kanada, Ufaransa, Ujerumani na Italia, ni washirika wa jumuiya hiyo iliyoundwa kukabiliana na kitisho cha kambi ya Mashariki, maarufu kama Warsaw, iliyokuwa ikiongozwa na Urusi wakati wa Vita Baridi duniani.