Umoja wa Mataifa wataka kuchunguza mauwaji ya Mali
11 Aprili 2022Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwenye ukanda wa Sahel, El-Ghassim Wane, ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa mamlaka nchini Mali bado haijaruhusu uchunguzi wa Umoja wa Mataifa ya licha ya mazungumzo ya kina na viongozi hao.
''Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitafuta ufikiaji wa eneo hilo na uliweza kufanya uchunguzi wa safari ya ndege mnamo Aprili 3. Idhini ya kuwasilisha tume ya pamoja bado haijatolewa. Tunafuatilia ushirikiano wetu wa kina na mamlaka ya kitaifa ili kutatua tatizo hili."
Jeshi la Mali lilitangaza mnamo Aprili 1 kwamba limewaua wanamgambo 203 huko Moura, katikati mwa Mali, wakati wa operesheni mwishoni mwa mwezi Machi. Hata hivyo, tangazo hilo lilifuatia ripoti za mitandao ya kijamii zilizosambazwa kwa wingi kuhusu mauaji ya raia katika eneo hilo.
Soma pia :HRW: Jeshi la Mali liliwaua watu 300 mwezi Machi
Tuhuma za mauwaji ya maksudi
Shirika la kimataifa la kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema wiki hii kwamba jeshi la Mali liliua raia takriban 300 katika mji wa Moura. Shirika hilo limeripoti kuwa baadhi ya watu katika mji wa Moura, ambao wanajeshi waliwachukulia kuwa wapiganaji wa itikadi kali, waliuawa kwa maksudi. Eneo hilo ni moja ya maeneo yanayokabiliwa na vurugu kubwa katika kanda ya Sahel.
El-Ghassim Wane amesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, umeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya mashambulizi ya kiholela dhidi ya raia, kukamatwa kwa watu kinyume cha sheria, mauaji, unyanyasaji na kutoweka kwa lazima katikati mwa Mali tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Urusi imetoa kile kinachoelezwa rasmi kama wakufunzi wa kijeshi kwa Mali, ambayo imekuwa ikipambana na mzozo wa kikatili wa wanajihadi tangu mwaka 2012. Marekani, Ufaransa na nchi nyingine za Magharibi zinasema wakufunzi hao ni wahudumu wa kampuni ya ulinzi ya kibinafsi ya Urusi ya Wagner.
Soma piaUN yaelezea hofu juu ya vurugu katika kanda ya Sahel:
Serikali ya tangaza kuanzisha uchunguzi wake
Akiashiria kuongezeka kwa visa vya ukiukaji wa haki za binaadamu, Richard Mills, naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, aliliambia Baraza hilo kwa nini Marekani inaendelea kuonya nchi dhidi ya kushirikiana na kundi la Wagner lenye uhusiano na serikali ya Urusi.
Umoja wa Mataifa uliikaribisha taarifa kutoka Mali kwamba mahakama ya kijeshi imefungua uchunguzi kuhusu matukio ya Moura. Hata hivyo, umeiomba mamlaka ya Mali itoe ushirikiano unaohitajika kwa tume ya MINUSMA kufikia eneo la ukiukwaji unaodaiwa.