Umoja wa Mataifa wataka mapigano yasitishwe Yemen
5 Desemba 2017Idadi ya watu waliofariki katika mapigano hayo nchini Yemen katika muda wa karibu wiki moja sasa imepanda na kufikia watu 234 na wengine 400 wamejeruhiwa, shirika la kimataifa la msalaba mwekundu ICRC imesema leo.
Mji mkuu wa Yemen Sanaa ulikuwa kimya leo baada ya siku tano za mapigano ambayo yalifikia kilele kwa kifo cha rais wa zamani wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh, hata hivyo ndege za shirika la msalaba mwekundu na Umoja wa mataifa zimetua katika uwanja wa ndege wa mjini Sanaa.
Mapigano ya mitaani katika mji mkuu yalisita licha ya mashambulizi karibu 25 ya anga yaliyofanyika usiku, mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa mataifa nchini Yemen Jamie McGoldrick amesema.
Mazishi ya rais wa zamani wa Yemen yanatarajiwa kufanyika leo. Aliuwawa na washirika wake wa zamani wa Kihuthi siku ya Jumatatu , siku mbili baada ya kutangaza kwamba anachukua msimamo tofauti na kujitoa kutoka muungano na Wahuthi katika vita hivyo na kwamba anapanga kupingana nao.
Upungufu wa chakula
Washirika wa familia yake walipambana na Wahuthi tangu wiki iliyopita, hali ambayo ni mabadiliko makubwa katika mzozo huo ambapo kwa kiasi kikubwa kulikuwa na mkwamo kwa muda mwingi wa miaka mitatu iliyopita.
Umoja wa mataifa unasema upungufu wa chakula uliosababishwa na mapigano ya makundi hayo ulisababisha kuzuwia upelekaji wa chakula na kusababisha mzozo mbaya kabisa wa kiutu kuwahi kuonekana duniani. Mamilioni ya watu huenda watafariki kwa njaa kali kabisa wakati huu.
"Watu wanajitokeza hivi sasa wakitoka majumbani mwao baada ya siku tano za kujifungia kama wafungwa," amesema McGoldrick alipokuwa akitoa maelezo kwa kikao cha Umoja wa Mataifa, akizungumza kwa simu kutoka mjini Sanaa.
"Wanatafuta mahali salama, wakihamisha familia zao iwapo mambo yatacharuka tena na wakati huo huo wakitafuta matibabu na kujaribu kuwatuliza watoto wao ambao wametaharuki baada ya siku tano za mashambulizi makali ya makombora, risasi na mashambulizi ya anga."
Mashambulizi ya anga usiku yameshambulia majengo ya serikali, makaazi ya rais na madaraja , na watu hivi sasa walikuwa wanajiweka tayari iwapo mapigano zaidi yatazuka ama mashambulizi ya anga yataendelea, McGoldrick , alisema, akielezea hali kuwa isiyotabirika kabisa".
Robert Mardini , mkurugenzi wa shirika la kimataifa la msalaba mwekundu kwa ajili ya mashariki ya kati , pia aliandika katika ukurasa wa Twitter , kwamba " "vikosi vyetu vya shirika la msalaba mwekundu hivi sasa vinafanya kila linalowezekana kupeleka madawa katika hospitali , vifaa vya upasuaji na mafuta kwa ajili ya magari.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman