1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Nchi zinahitaji utayari kufanikisha makubaliano COP29

Angela Mdungu
21 Novemba 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mataifa yanapaswa kuwa na utayari ili kupata makubaliano kuhusu ufadhili wa kifedha wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: Andrea Renault/AFP/Getty Images

Guterres ameyasema hayo katika mazungumzo yanayoelekea kukwama kwenye mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi unaofanyika mjini Baku, Azerbaijan.

Akizungumza katika mkutano huo wa mabadiliko ya tabianchi COP29 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hakuna nafasi ya mazungumzo hayo kushindwa kupata makubaliano. Ametoa mwito huo wakati  mataifa yakikabiliwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu masuala muhimu, huku siku moja pekee ikiwa imesalia kabla ya mkutano huo kufikia ukingoni Ijumaa.

Akihutubia mkutano huo Guterres amesema, "Ninahisi kiu ya makubaliano, lakini masuala mgongano yanajitokeza. Lakini na tuwe wakweli, tofauti nyingi kubwa bado zipo. Bado hakuna uhakika wa mafanikio. Tunahitaji msukumo mkubwa ili kuifikisha mwisho mijadala. Ili kutoa makubaliano yaliyokamilika yenye usawa kuhusu masuala yaliyosalia, yenye malengo mapya ya ufadhili. Tusiruhusu kushindwa."

Guterres ameongeza kuwa kama makubaliano hayatafikiwa, huenda mipango ya kila nchi kuhusu mazingira ikawa hatarini.  Mpasuko mkubwa baina ya nchi zinazoshiriki katika mkutano huo wa Cop29,  umejitokeza wazi Alhamisi baada ya kutolewa kwa rasimu ya makubaliano inayohusu namna ya kuzifadhili nchi masikini katika kukabiliana na athari za ongezeko la joto duniani na kuelekea uchumi wa kijani.

Soma zaidi: Dunia bado imegawanyika kuhusu fedha wakati muda ukiyoyoma COP29

Miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa kuwa hayakuainishwa katika rasimu hiyo ni pamoja na ni nani wa kufadhili mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na namna fedha za ufadhili zitakavyopatikana.

Mkutano wa COP29, Baku, ArzebaijanPicha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Kando ya mgawanyiko kuhusu fedha, mataifa mengi yamesema kuwa rasimu hiyo imeshindwa kuakisi sababu ya uharaka wa kuyaondoa matumizi ya makaa, mafuta na gesi, nishati zinazohusika pakubwa kusababisha ongezeko la joto duniani.

Marekani yaonesha wasiwasi kutokana na rasimu kukosa uwiano

Kutokana na tofauti hizo, Marekani imesema ina wasiwasi mkubwa unaotokana na kukosa uwiano kwa rasimu ya makubaliano iliyotolewa katika mkutano huo. Mjumbe maalumu wa tabianchi wa Marekani John Podesta amesema  ni muhimu sana kwa mkutano huo kukubali maamuzi magumu katika masuala yote yanayohusu ajenda ya tabianchi.

Kwa upande wake Uingereza imetoa wito kwa nchi kuendelea kuzingatia makubaliano ya kimataifa kuhusu kuondokana na nishati ya visukuku. Saudi Arabia kwa upande imeonya kuwa haitakubali mkataba wowote unaozilenga sekta maalumu ikiwemo nishati ya visukuku.

Nayo China, imeungana na mataifa mengine katika kuikataa rasimu ya ufadhili wa  mabadiliko ya tabianchi lakini imeyaomba kuondoa tofauti zao. Mjumbe wa serikali ya China  Xia Yingxian amesema rasimu iliyotolewa ina vipengele ambavyo havikubaliki kwa nchi yake.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW