1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Umoja wa Mataifa wataka mivutano zaidi izuiwe

17 Novemba 2022

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuzuiwa kwa mivutano zaidi baada ya kombora kushambulia kijiji cha Poland karibu na mpaka wa Ukraine na kuwaua watu wawili.

Polen, Przewodow | Raketeneinschlag nahe der ukrainischen Grenze
Picha: Jakub Orzechowski/Agencja Wyborcza.pl/REUTERS

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani mkuu wa masuala ya kiusalama na kujenga amani katika Umoja wa Mataifa, Rosemary DiCarlo amesema shambulizi hilo la Jumanne lilikuwa kitisho kinachokumbusha umuhimu wa kuzuia mivutano zaidi.

''Kadri vita vinavyoendelea, hatari ya uwezekano wa kutokea majanga zaidi inakuwa ya kweli. Tukio la juzi Poland karibu na mpaka wa Ukraine, lilikuwa linatukumbusha haja ya kuzuia mapigano zaidi,'' alisisitiza DiCarlo.

DiCarlo amebainisha kuwa mashambulizi mengi yaliyofanywa tangu Urusi iivamie Ukraine Februari 24 yanaweza kuifanya hali kuwa mbaya zaidi katika miezi ijayo wakati wa majira ya baridi. Amesema mashambulizi yanayowalenga raia na miundombinu ya raia yanakiuka sheria za kimataifa, huku akisisitiza kwamba mapigano makali bado yanaendelea mashariki mwa majimbo ya Donetsk na Luhansk.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vasily NebenziaPicha: picture alliance / NurPhoto

Kwa upande wake, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield anasema huku wakiwa bado hawajui ukweli wote kuhusu shambulizi la Poland, wanajua kitu kimoja. Anasema janga hilo lisingetokea kamwe, lakini limetokea kutokana na uvamizi usio wa lazima wa Urusi nchini Ukraine na makombora yake ya hivi karibuni dhidi ya miundombinu ya raia.

Urusi yazishutumu Ukraine na Poland

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzia amezishutumu Ukraine na Poland kwa kutaka kuanzisha mzozo wa moja kwa moja kati ya Urusi na Jumuia ya Kujihami ya NATO. Aidha, wawakilishi wa China na India kwa mara nyingine tena wametoa wito wa kumalizwa kwa ghasia.

Wakati huo huo, Marekani na washirika wake wa Magharibi wametupiana lawama na Urusi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu shambulizi la Poland lilivyoshughulikiwa. Marekani na Albania zimetoa wito kwa baraza hilo kutoa taarifa za hali ilivyokuwa Ukraine wiki iliyopita, huku mkutano huo ukigubikwa na shambulizi la Poland lililowaua wakulima wawili.

Rais wa Poland, Andrzej DudaPicha: Pawel Supernak/PAP/dpa/picture alliance

Huku hayo yakijiri Ukraine inaweza kupata ruhusu ya kwenda kusini mashariki mwa Poland ambako shambulizi hilo limetokea. Hayo yameelezwa Alhamisi na Jakub Kumoch, mshauri wa ngazi ya juu wa sera za kigeni wa Rais wa Poland, Andrzej Duda, baada ya Ukraine kutoa ombi la kuruhusiwa kulizuru eneo hilo. Hata hivyo, siku ya Jumatano Rais Duda alisema ruhusu kwa Ukraine kulizuru eneo hilo, kutahitaji makubaliano ya nchi zote mbili zinazoongoza uchunguzi huo, ambazo ni Poland na Marekani. Kumoch amesema timu ya wachunguzi wa Poland na Marekani tayari wako kwenye eneo hilo.

Mashambulizi ya anga ya Urusi yaua watu 11 

Katika eneo la mapambano kwenyewe, maafisa wa Ukraine wamesema mashambulizi ya anga ya Urusi yamewaua watu wapatao wanne na kuwajeruhi wengine 11. Mashambulizi hayo yameharibu miundombinu ya nishati, majengo ya makaazi na eneo la viwanda. Aidha, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine, Denys Monastyrsky amesema polisi wa Ukraine imesema wamepata ushahidi wa madai ya uhalifu, ikiwemo utesaji katika eneo lililokombolewa la Kherson.

Ama kwa upande mwingine, afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa anayehusika na mazungumzo ya kusafirisha nafaka kutoka Ukraine kupitia bandari za Bahari Nyeusi, Alhamisi amepongeza makubaliano yaliyofikiwa ya kuurefusha mpango huo.

(AFP, DPA, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW