1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka Saudi Arabia iwajibishwe

21 Oktoba 2018

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, mashirika ya kutetea haki za binadamu na vyama vya waandishi wa habari vimetaka waliohusika na mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi nchini Uturuki waadhibiwe.

Jamal Khashoggi
Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Guterres amesema amepata wasiwasi mkubwabaada ya Saudi Arabia kukiri kuwa Khashoggi alifikwa na umauti kwenye ubalozi wake mdogo. katibu mkuu wa Umoja wa mataifa  ameongeza kusema kuwa kuna haja ya kufanyika uchunguzi wa haraka na wa kina kuhusiana na kadhia hiyo ili waliohusika wachukuliwe hatua. Uturuki imeelezea kutokufurahishwa nanhatua ya Saudi Arabia ya kuchelewa kukiri kwamba imehusika na mauaji ya Khashoggi na kukitaja kitendo hicho kuwa cha kufedhehesha.

Shirika la Amnesty International limesema maelezo ya Saudi Arabia kuhusu mauaji ya Khashoggi yanaonekana kufunika mauaji ya kinyama,na taarifa nyingine mbaya zinazodhihirisha  kwamba Saudi Arabia inakiuka haki za binadamu. Shirika hilo la Amnesty International limeitaka nchi hiyo kuutoa mwili wa mwandishi huyo wa habari ili ufanyiwe uchuguzi kubainisha chanzo cha kifo chake.

Taarifa ya vyombo vya habari vya serikali nchini Saudi Arabia imeongeza kusema kuwa mshauri wa mahakama ya Saudi Arabia, Saud al-Qahtani na naibu Mkuu wa idara ya upelelezi Ahmed Asiri wamefukuzwa kazi.

Trump aikingia kifua Saudia Arabia

Kabla ya Saudi Arabia kutoa taarifa hiyo, rais wa Marekani Donald Trump alisema anaweza kuzingatia kuiwekea vikwazo Saudi Arabia lakini wakati huo huo amesisitiza umuhimu wa uhusiano wa nchi hizo mbili. Trump amesema maelezo yaliyotolewa na Saudi Arabia ni ya kuaminika.

Mwana mfalme Mohammed bin SalmanPicha: picture-alliance/empics/V. Jones

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Saudi Arabia (SPA) mabishano kati ya Jamal Khashoggi na watu aliokutana nao kwenye ubalozi huo mdogo yaligeuka na kuanza kurushiana makonde ugomvi ambao ulisababisha kifo chake.

Hata hivyo Saudi Arabia haikutoa ushahidi wa kuunga mkono maelezo yake kuhusu hali halisi ilivyokua na haijulikani kama washirika wake wa Magharibi wataridhishwa na maelezo yaliyotolewa na Saudi Arabia. Mkasa wa kutoweka mwandishi huyo wa habari ulisababisha kilio kutoka kwa jamii ya kimataifa na pia kuleta hali ya mvutano kati ya Saudia na nchi za magharibi. Uchunguzi bado unaendelea lakini hadi sasa raia 18 wa Saudi wamekamatwa.

Taarifa ya vyombo vya habari vya serikali nchini Saudi Arabia imeongeza kusema kuwa mshauri wa mahakama ya kifalme Saud al-Qahtani na naibu Mkuu wa idara ya upelelezi Ahmed Asiri wamefukuzwa kazi. Kabla ya Saudi Arabia kutoa taarifa hiyo mapema leo, rais wa Marekani Donald Trump alisema anaweza kuzingatia kuiwekea vikwazo Saudi Arabia lakini wakati huo huo amesisitiza umuhimu wa uhusiano wa nchi hizo mbili.

Uturuki yatishia kuanika kila kitu kweupe

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. Ernst

Vyombo vya habari vya serikali ya Uturuki vimekuwa vikidai mara kwa mara kwamba Khashoggi aliteswa na kuuuawa na kuchinjwa na kikosi cha makatili wa Saudi Arabia ndani ya ubalozi, lakini Uturuki bado haijafafanua maelezo kamili kuhusu uchunguzi wake.

Saudi Arabia hapo awali ilizikanusha tuhuma kwamba Khashoggi aliuawa katika ubalozi wake mdogo na kuzitaja tuhuma hizo kuwa hazina maana. Vyombo vya habari vya serikali ya Saudi Arabia pia vilipuuza madai kutoka kwa maofisa wa Uturuki kuwa kikosi cha Saudi "cha mauaji," ikiwa ni pamoja na afisa mmoja kati ya washirika wa ndani wa mwana mfalme Mohammed bin Salman na mtaalam wa kuchunguza maiti  kilikwenda mapema na kumsubiri Khashoggi ndani ya ubalozi huo mdogo mjini Istanbul.

Muda mfupi kabla ya tangazo la Saudi Arabia, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Mfalme Salman walikubaliana kupitia njia ya simu kuendelea kushirikiana katika uchunguzi wa kutoweka kwa Khashoggi. Msemaji wa ikulu ya Marekani Sarah Huckabee Sanders amesema Marekani imesikitishwa na uthibitisho wa kifo cha Jamal Khashoggi, na amewatumia rambirambi familia yake, mchumba na marafiki zake.

Khashoggi, aliyekuwa mkosoaji mkuu wa sera ya mwana mfalme Mohammed bin Salman, alitoweka baada ya kuingia ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul mnamo tarehe 2 mwezi huu kwa ajili ya kupata hati ambayo ingelimwezesha kufunga ndoa na mchumba wake wa Kituruki.

Mwandishi:Zainab Aziz/RTRE/p.dw.com/p/36res

Mhariri: Yusra Buwayhid

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW