1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka uchunguzi huru kadhia ya Bobi Wine

29 Agosti 2018

Umoja wa Mataifa unataka uchunguzi huru juu ya machafuko yaliyoikumba Uganda baada ya kukamatwa na kuteswa kwa wabunge kadhaa, akiwemo nyota wa zamani wa muziki, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.

Uganda - Bobi Wine (Sänger) mit Krücken in Gerichtssaal in Gulu
Picha: Getty Images/AFP

Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein, aliitolea wito serikali ya Rais Yoweri Museveni kuhakikisha unafanyika uchunguzi huru juu ya ghasia hizo, yakiwemo madai ya mauaji ya makusudi, matumizi ya nguvu kupita kiasi na mateso yaliyofanywa na polisi.

"Ninatiwa wasiwasi hasa na tuhuma kwamba vikosi vya usalama vimewatesa na kuwatendea vibaya mahabusu. Tumepokea pia taarifa za namna mauaji yalivyofanyika na ukamatwaji ovyo ovyo dhidi ya raia wakati wa maandamano." Alisema Zeid wakati akizungumza na waandishi mjini Geneva siku ya Jumatano (Agosti 29).

Zeid, ambaye muda wake wa kuhudumu kama mkuu wa kamisheni hiyo unamalizika Ijumaa, alisimulia taarifa zilizofikishwa ofisini pake zinazochambua matukio ya nchini Uganda kama yalivyoanza kujiri tarehe 13 mwezi huu nchini Uganda.

Siku hiyo, dereva wa mbunge Kyagulanyi alipigwa risasi na kuuawa akimsubiri bosi wake kwenye maegesho ya magari mjini Arua, huku polisi ikimkamata mbunge huyo na wenziwe watatu, mbunge mmoja mstaafu na mbunge mwengine mteule waliokuwa kwenye chumba cha hoteli.

Kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, watu wengine 28 walikamatwa, wakiwemo waandishi wawili wa habari na wanawake wawili.

Zeid Ra'ad Al Hussein, mkuu wa kamisheni ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa anayemaliza muda wake ataka uchunguzi huru mkasa wa Bobi Wine.Picha: Reuters/P. Albouy

Mbunge Kyagulanyi, ama Bobi Wine, aliachiwa kwa dhamana juzi Jumatatu baada ya wiki mbili za kuwekwa kizuizini, akitarajiwa kurejea tena mahakamani hapo kesho, Alhamisi.

Bobi Wine auguwa figo

Mwanamuziki huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa anakabiliwa na mashitaka ya uhaini, sambamba na wenziwe 33 wakiwemo wabunge wengine wawili, katika kesi ambayo imekosolewa vikali kimataifa.

Hayo yakiendelea, taarifa kutoka Uganda zinasema kuwa Bobi Wine ana tatizo la figo, ambalo linahitaji kushughulikiwa kwa haraka nje ya nchi hiyo, kwa mujibu wa wakili wake, ambaye amezungumza leo na waandishi wa habari, siku mbili baada ya mwanasiasa huyo kuachiwa kwa dhamana.

Wakili Medard Sseggona ameliambia shirika la habari la AP kwamba ripoti ya daktari huru inaonesha kuwa mteja wake anauguwa maradhi ya figo. Taarifa zaidi zinasema kuwa akiwa mikononi mwa vyombo vya dola, mbunge huyo alipigwa na kuvunjwa mbavu pamoja na kuvutwa uume wake. 

Tangu achaguliwe kuwa mbunge mwaka jana, Bobi Wine amejipatia umashuhuri mkubwa ndani na nje ya nchi yake kwa kuwapigia kampeni wagombea wa upinzani ambao kila mara hushinda kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupambana na Rais Museveni, mmoja kati ya marais wa muda mrefu kabisa barani Afrika.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga