1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka ulimwengu kuisaidia Afghanistan

16 Agosti 2021

Wawakilishi wa serikali ya Afghanistan na wanamgambo wa Taliban wako katika mchakato wa kufanya mazungumzo baada ya kundi hilo kuudhibiti mji mkuu Kabul huku Umoja wa Mataifa ukitaka ulimwengu kuisadia Afghanistan.

Afghanistan | ehemaliger Präsident Hamid Karzai
Picha: Mariam Zuhaib/AP Photo/picture alliance

Wawakilishi wa serikali ya Afghanistan iliyosambaratika pamoja na wanamgambo wa Taliban wako katika mchakato wa kufanya mazungumzo baada ya kundi hilo kuudhibiti mji mkuu Kabul na kuzua sintofahamu kubwa ndani na nje ya taifa hilo huku Umoja wa Mataifa ukiutaka ulimwengu kushirikiana ili kupambana na kitisho cha kimataifa cha ugaidi nchini humo.

Msemaji wa rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai, Yousuf Saha ameliambia shirika la habari la DPA kwamba mkakati huo unaendelea. Amesema, awali walisisitiza kuhusu umuhimu wa kulinda maisha na mali za watu. Hata hivyo hakukua na tamko lolote kutoka kundi la Taliban.

Hata hivyo bado haiko wazi wakati gani mazungumzo hayo yatafanyika na hata iwapo kundi la Taliban lina mpango wowote wa kufanya mashauriano. Baada ya rais Ashraf Ghani kukimbia Afghanistan wakati kundi hilo lilipokaribia kuuzingira mji mkuu Kabul, taifa hilo sasa liko chini ya baraza maalumu linaloratibu makabidhiano ya mamlaka kwa Taliban.

Baraza hilo linawahusisha rais huyo wa zamani Karzai, mwenyekiti wa baraza la juu la maridhiano ya kitaifa, Abdullah Abdullah na mbabe wa zamani wa kivita Gulbuddin Hekmatyar.

Rais wa Marekani Joe Biden anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kufuatia Taliban kuiangusha serikali ya KabulPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Huku hayo yakiripotiwa, rais Joe Biden wa Marekani anatarajiwa hivi karibuni kuzungumzia hatua hiyo ya Taliban, hii ikiwa ni kulingana na mshauri wa masuala ya usalama wa taifa kwenye ikulu ya White House Jake Sullivan, wakati akikabiliwa na ukosoaji mkali baada ya Taliban kuiangusha serikali.

Sullivan amekiambia kituo cha utangazaji cha ABC kwamba, Wamarekani wana shauku ya kusikia kile atakachokisema rais wao na kuongeza kuwa kwa sasa anajadiliana kwa karibu na timu ya usalama wa taifa. Hata hivyo hakusema ni lini hasa Biden atazungumza.

Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan amezungumzia hatua hiyo ya Taliban kuidhibiti Afghanistan akisema taifa hilo hatimaye limejifungua kutoka kwenye minyororo ya utumwa baada ya kumalizika kwa vita vya miaka 20 bila ya machafuko.

Alisema "Unapokuwa mtumwa wa fikra, basi kumbuka kwamba utumwa wa kifikra ni mbaya zaidi kuliko utumwa wenyewe. Ni vigumu kukata minyororo ya utumwa wa fikra. Kule Afghanistan wamekata minyororo ya utumwa, lakini mnyororo wa utumwa wa fikra haukatiki. Unatakiwa uvae nguo wanazovaa na kuendana na mitindo yao kwa sababu unadhani wao ni zaidi yako na utumwa wa fikra kamwe hauwezi kufanikisha chochote kikubwa."

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aiomba jamii ya kimataifa kusaidia kupambana na kitisho cha ugaidi Afghanistan Picha: Javier Soriano/AFP

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito kwa ulimwengu kushirikiana katika kupambana na kitisho cha ugaidi nchini humo. Guterres ameuambia mkutano wa dharura wa baraza la usalama la umoja huo kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuhakikisha Afghanistan haiwi tena jukwaa ama eneo litakalotumiwa na makundi ya kigaidi kuendeleza shughuli zao.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kijihami ya NATO Jens Stoltenberg anataraji kuongoza kikao cha dharura kesho kuhusiana na hali nchini Afghanistan na baadae kuzungumza na waandishi wa habari.

Huko Qatar, waziri wa mambo ya kigeni Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani, amewaambia waandishi wa habari mjini Doha kwamba  wanafanya juhudi za kusaidia kuwarejesha nyumbani wanadiplomasia wake na watumishi wa kigeni kwenye mashirika ya kimataifa wanaotaka kuondoka Afghanistan. Qatar imekuwa na jukumu kubwa la kufanikisha makubaliano ya kisiasa nchini Afghanistan tangu mwaka 2013.

Nchini Ujerumani, kiongozi wa chama cha kansela Angela Merkel cha CDU, Armin Laschet amesema kuondoka kwa vikosi vya NATO nchini Afghanistan ni pigo kubwa kwa jumuiya hiyo tangu ilipoundwa na kuongeza kuwa uvamizi huo wa kimataifa haukufanikiwa na baadhi ya wachambuzi wakisema Afghanistan ni janga kwenye sera za kigeni za Marekani.

Mashirika: RTRE/AFPE/AFP/DW