1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na hali Burundi

Admin.WagnerD9 Juni 2015

Burundi imekataa matakwa ya vyama vya upinzani ya kumtaka Rais Pierre Nkurunziza kutogombea muhula wa tatu huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa nchi hiyo iko katika hatari ya kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe

Picha: Reuters/G. Tomasevic

Msemaji wa serikali ya Burundi Philippe Nzobonariba amesema uamuzi wa wa Rais Nkurunziza kugombea muhula wa tatu ni jambo lisilojadilika na kupuuzilia mbali miito kutoka kwa wanasiasa wa upinzani ya kumtaka Rais huyo kuachia madaraka.

Serikali ya Burundi imesema pendekezo la tume ya uchaguzi nchini humo kuahirisha uchaguzi wa rais hadi tarehe 15 mwezi ujao itakuwa ni wa mwisho.

Hayo yanakuja wakati mkuu wa kamisheni ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa akionya kuwa kuongezeka kwa ghasia zinazofanywa na kundi la vijana wenye silaha walio watiifu kwa serikali ya Burundi ikiwemo mauaji, utekaji nyara na mateso kunatishia kuliyumbisha zaidi taifa hilo la Afrika Mashariki.

Uchu wa madaraka utaiweka Burundi pabaya

Zeid Ra'ad Al Hussein amesema kitu cha mwisho taifa la Burundi linahitaji baada ya kujenga amani kwa muongo mmoja uliopita ni kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kwasababu ya uchu wa watu walio wachache kutaka kusalia au kupata madaraka kwa kutumia kila namna.

Mkuu wa kamisheni ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al HusseinPicha: picture-alliance/dpa/S. Di Nolfi

Zeid ameelezea kushutushwa na madai ya kila mara kuwa wapiganaji wa kundi lijulikanlo Imbonerakure lenye mafungamano na tawi la vijana la chama tawala Burundi cha CNDD FDD wanafanya mashambulizi wakipewa maagizo na chama hicho, polisi,na mashirika ya kijasusi kwa kuwapa silaha, magari na wakati mwingine hata sare.

Umoja wa Mataifa umesema iwapo madai hayo yana ukweli wowote, basi yanaashiria kuwepo njama hatari mno za kuzidisha hali ya taharuki na uoga nchini Bunrundi na kuifanya hali ambayo tayari ni tete kuwa mbaya zaidi.

Takriban raia laki moja wa Burundi wametorokea nchi jirani wakihofia usalama wao lakini Nzobonariba amesema wengi wa waliotoroka wamefanya hivyo kwasababu ya uvumi unaosambazwa na wanasiasa wasio taka kuwepo chaguzi wakisaidiwa na raia wa kigeni na mashirika yasio ya serikali yanayotaka kuisukuma nchi hiyo kuelekea kuwa na ghasia.

Wanasiasa wanaompinga Nkurunziza wanasisitiza kuwa kugombea kwake muhula wa tatu ni kinyume na katiba ya nchi hiyo na mkataba wa amani wa Arusha uliofikiwa mwaka 2006.

Kalenda mpya ya uchaguzi yapingwa

Vyama vya upinzani vimepinga kalenda mpya ya chaguzi vikisema mazingira ya kuandaa chaguzi huru na haki hayajazingatiwa. Kiongozi wa chama kimoja cha upinzani Charles Nditije ametaka kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi kusimamia chaguzi hizo. Nditije ametaka pia wapiganaji wa kundi la Imbonerakure kupokonywa silaha.

Waandamanaji wakiandamana katika mji wa Ijenda wakipinga utawala wa NkurunzizaPicha: Reuters/G. Tomasevic

Umoja wa Mataifa, nchi za magharibi na Umoja wa Afrika zimekuwa zikishinikiza pande zote mbili zinazozana nchini humo kuutatua mzozo huo kupitia mazungumzo lakini duru kadhaa za mazungumzo zimeshindwa kufikia suluhu.

Baadhi ya wanasiasa wa upinzani na makundi ya asasi za kiraia zimemshutumu mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayesimamia mazungumzo hayo Said Djinnit kwa kuegemea upande mmoja madai ambayo maafisa wa Umoja wa Mataifa wameyakanusha.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu