1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waunda Jukwaa la kupambana na ubaguzi

Saleh Mwanamilongo
3 Agosti 2021

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeunda jukwaa jipya la watu wenye asili ya Afrika ambao kwa karne kadhaa wamekumbwa na machungu ya ubaguzi duniani kote.

Umoja wa Mataifa launda Jukwaa jipya la watu wenye asili ya Afrika
Umoja wa Mataifa launda Jukwaa jipya la watu wenye asili ya AfrikaPicha: Rick Bajornas/UN/Xinhua/picture alliance

Azimio hilo lilipitishwa kwa kauli moja na wajumbe wote 193 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Lengo la Jukwaa hilo pia ni kuboresha usalama na hali ya maisha ya watu wa asili ya Afrika na maingiliano yao kikamilifu katika mahali wanakoishi.

 Jukwaa la Kudumu la Watu wa Asili ya Afrika, litakuwa ni bodi ya ushauri ya watu 10 ambao watashirikiana na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lenye makao makuu huko Geneva, Uswisi. Jukwaa hilo linalenga kutambuliwa, sheria na maendeleo ya watu wa asili ya Afrika duniani kote.

Kupitia azimio lililopitishwa jana Jumatatu, ambalo linaeleza kinagaubaga mamlaka na majukumu ya chombo hicho kipya, Baraza Kuu linapazia sauti kuenea kwa harakati za misimamo mikali yenye kibaguzi duniani kote na kuelezea masikitiko yake juu ya kuendelea kushamiri kwa vitendo hivyo.

Ubaguzi wa rangi bado sugu duniani kote

Ubaguzi wa rangi unakiuka katiba ya UN na msingi wa maadili yakePicha: BRENDAN SMIALOWSKI/AFP

 Kuundwa kwa jukwaa hilo kumekuja siku chache kabla ya madhimisho ya miaka 20 ya Kongamano la Dunia dhidi ya Ubaguzi wa rangi lililofanyika Septemba 2001 nchini Afrika ya Kusini.

 Hatua ya hivi sasa imekuja siku chache baada ya Baraza la Haki za Binadamu kuanzisha jopo la wataalamu wa kuchunguza mifumo ya kibaguzi katika taasisi za kipolisi kwa watu wenye asili ya Afrika.

Azimio hilo la Jumatatu limesema licha ya juhudi za kupambana na ubaguzi wa rangi,vitendo vya kibaguzi, chuki dhidi ya wageni, lakini hali hiyo inaendelea kuwepo na vitendo hivyo vinatakiwa kulaaniwa.

Jopo la watu kumi

Jukwaa pia litakuwa chombo cha kukusanya mifano boraPicha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Baraza Kuu la Umoja wa Mtaifa limesema watu wote walizaliwa huru na wanahaki sawa na wanauwezo wa kuchangia ujenzi na maendeleo ya jamii zao. Azimio la baraza hilo limetowa wito wa kupambana na ubaguzi wa rangi duniani kote na kusema ni suala la kipaumbele kwa kumuiya ya kimataifa.

Miongoni mwa majukumu ya Jukwaa hilo ni kusaka ujumuishaji kamilifu wa watu wenye asili ya Afrika kiuchumi, kisiasa na kijamii katika jamii ambako wanaishi. Na wapate haki hizo kama raia wengine bila ubaguzi na wafurahie haki za binadamu.

Jukwaa la Kudumu la Watu wa Asili ya Afrika, litakuwa na wajumbe watano watakaochaguliwa na serikali zao na kisha kupigiwa kura na Baraza Kuu. Kisha wajumbe wengine watano watakaochaguliwa na Baraza la Haki za Binaadamu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW