1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wauongezea muda ujumbe wa amani Darfur.

1 Novemba 2019

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limepiga kura ya kuviongezea muda wa mwaka mmoja zaidi vikosi vya pamoja vya usalama vya Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika katika jimbo la Magharibi mwa Sudan la Darfur.

UN Mission UNAMID
Picha: picture-alliance/dpa/S. Price

Juhudi kubwa zinaendelea kufanywa na Umoja wa mataifa ili kuhakikisha amani endelevu na hali ya utulivu inapatikana katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur.

Azimio lililodhaminiwa na Uingereza pamoja na Ujerumani limemtaka katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuwasilisha ripoti na mapendekezo kwa baraza hilo mnamo Januari tarehe 31 kutathmnini hali ilivyo Darfur.

Naibu balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Jonathan Allen amesema ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ujulikanao kwa kifupi kama UNAMID unalo jukumu muhimu la kuweka mazingira mazuri ya amani na maridhiano hasa wakati huu wa mchakato wa amani. Mwanadiplomasia huyo ameongeza kuwa kwa kuongeza muda kwa vikosi vya UNAMID Umoja wa Mataifa umetambua umuhimu wake katika kudumisha hali ya utulivu katika jimbo la Darfur."

Vikosi vya UNMID vikiwa kwenye shughuli zake za kawaida huko DarfurPicha: picture-alliance/dpa/A. Gonzales

Mnamo mwisho wa mwezi Juni baraza la usalama la umoja wa mataifa pia lilikubaliana kutoondoa ujumbe wa UNAMID hadi Oktoba 31. Baada ya hapo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika walipendekeza kuuongezea muda ujumbe huo hadi Oktoba 31 mwaka 2020, uamuzi ambao uliidhinishwa jana Alhamisi.

Julai mwaka jana baraza hilo la usalama pia lilipiga kura na kuamua kupunguza kwa idadi ya maafisa wa ujumbe wa UNAMID kufuatia hali ya utulivu kuanza kurudi na mizozo kupungua. Lengo lilikuwa ni kuviondoa kabisa vikosi hivyo ifikapo mwezi Juni tarehe 30 mwaka 2020.

Mzozo wa Darfur ulianza mwaka 2003 baada ya raia weusi nchini humo kuanzisha uasi dhidi ya serikali baada ya kudai kuwa serikali ya Sudan ilikuwa inaongozwa kwa misingi ya ubaguzi wa rangi na ukabila.

Pia Serikali ya Khartoum ilidaiwa kuwapa silaha wanamgambo wa Kiarabu kuwashambulia raia weusi, madai ambayo serikali iliyakanusha.

Mzozo wa Darfur uliendelea kwa muda wa miongo mitatu chini ya utawala wa aliyekuwa Rais Omar al-Bashirwakati ambao Sudan ilishuhudia umwagikaji wa damu sio tu katika jimbo la Darfur bali hata katika maeneo ya Blue Nile na Kordofan Kusini.

Utawala wa Al-Bashir uliangushwa mwezi Aprili mwaka huu baada ya maandamano makubwa kushuhudiwa nchini humo kushinikiza mabadiliko katika uongozi na baada ya hapo makubaliano ya kugawana madaraka yalitiwa saini mwezi Agosti kati ya jeshi na waandamanaji ambao waliitaka serikali kufikia makubaliano ya amani na makundi yenye silaha katika muda wa miezi sita.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW