UN yafichua majaribio ya mauaji dhidi ya viongozi ya Syria
12 Februari 2026
Ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres inaangazia kwa kina mazingira ya kiusalama nchini Syria na juhudi za makundi ya kigaidi kudhoofisha serikali mpya ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais Ahmad al‑Sharaa, Waziri wa Mambo ya Ndani Anas Hasan Khattab na Waziri wa Mambo ya Nje Asaad al‑Shibani walilengwa katika majaribio matano tofauti ya mauaji. Hata hivyo, hakuna shambulio lililofanikiwa.
Majaribio hayo ya mauaji yanadaiwa kufanywa na kundi linalojiita Saraya Ansar al‑Sunnah, ambalo linatajwa kuwa kibaraka wa kundi la Dola la Kiislamu IS.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa majaribio hayo ya mauaji ni ishara kwamba kundi la Dola la Kiislamu bado lina uwezo wa kupanga mashambulizi makubwa na lina nia ya kudhoofisha serikali mpya ya Syria kwa kutumia mianya ya kiusalama na mazingira ya kutokuwa na uhakika nchini humo.