1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiChina

UN yasema "sheria kandamizi" zinatumika mkoa wa Xinjiang

28 Agosti 2024

Ofisi ya OHCHR imesema "sheria kandamizi " zinaendelea kutumika nchini China, miaka miwili baada ya kutolewa ripoti iliyotaja uwezekano wa Beijing kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika mkoa wa Xinjiang.

Projektbilder Investigation | China | Hochsicherheitsanlage in Hotan
Kituo chenye ulinzi kinachoaminika kuwa kambi walimozuiliwa watu wa jamii ya waislamu walio wachache viungani mwa Hotan katika mkoa wa Xinjiang kaskazini magharibi mwa China.Picha: Greg Baker/AFP

China imeshtumiwa kwa kuhalalisha uwepo wa kambi za kuwafunga zaidi ya watu milioni moja wa jamii ya Uyghurs na jamii ya waislamu walio wachache katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Xinjiang - madai ambayo Beijing imeyakanusha vikali.

Umoja wa Mataifa umeeleza kwamba imefanya mazungumzo na maafisa wa China mjini Geneva tangu Februari mwaka jana 2023, ambayo yalifungua njia kwa Kamishna mkuu wa ofisi hiyo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Volker Türk kutuma timu kwenda Beijing kuanzia Mei 26 hadi Juni mosi mwaka huu.

Soma pia: UN: China huenda ilitenda uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Xinjiang

Msemaji wa OHCHR Ravina Shamdasani amewaambia waandishi wa habari kuwa timu hiyo ilifanya mazungumzo na mamlaka za China hasa juu ya sera zake za kukabiliana na ugaidi na mfumo wa haki jinai.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imehimiza kufanyika kile walichokiita "maendeleo ya wazi katika kuheshimu haki za binadamu China" pamoja na kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo mateso.