Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao
21 Julai 2020Viongozi hao walioonekana wenye uchovu wamekubaliana bajeti ya yuro trilioni 1.82 pia pamoja na hizo pesa za kufufua uchumi baada ya janga la virusi vya corona. Hatua hii imefikiwa kufuatia majadiliano ya siku nne ya usiku na mchana yaliyojawa na makabiliano na ubishi mkali kuhusiana na pesa na nguvu katika mojawapa ya mkutano wao mrefu zaidi wa kilele kuwahi kushuhudiwa.
Hizo bilioni 750 zitatolewa kama mkopo kwa nchi zilizoathirika vibaya zaidi na janga hilo huku makubaliano yakiafikiwa pia kuhusiana na bajeti hiyo ya miaka saba ya zaidi ya trilioni moja.
Mkutano ulitarajiwa kuisha Jumamosi
Charles Michel ni mwenyekiti wa mkutano huo wa kilele.
"Tumeonyesha imani kwa mustakabali wetu na makubaliano haya yanaonyesha kuwa Ulaya ni nguvu ya vitendo. Tumejadiliana kuhusu pesa ila makubaliano haya ni zaidi ya pesa. Naamini kwamba makubaliano haya yataonekana kama sehemu muhimu ya safari ya Ulaya," alisema Michel.
Mkutano huo wa kilele ulikuwa umepangiwa kufanyika kwa kipindi cha siku mbili ila kulilazimika kuongezwa siku mbili zengine kutokana na tofauti zilizokuwa baina ya viongozi wa nchi ishirini na saba za umoja huo.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen ameonyesha furaha yake kutokana na kuwa makubaliano ya mwaka huu hayakuwa baina ya nchi na nchi ila mataifa yameonyesha imani yake kwa halmashauri hiyo kuu. Von der Leyen amedai pia kwamba kama viongozi wanadhamiria kuleta mageuzi na uwekezaji zaidi Ulaya.
Makubaliano ya kihistoria
"Ninafurahi kwamba tumeweza kuyapata makubaliano haya na kufufuka kwa Ulaya kutakuwa kijani. Bajeti hii mpya itayapa nguvu makubaliano ya kijani ya Ulaya, itaongeza kasi ya uchumi wa Ulaya kuwa wa kidijitali na magauezi ya kitaifa yataongezwa. Tunaekeza kwa mustakabali wa Ulaya," alisema Von der Leyen.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameyataja makubaliano hayo kuwa ya kihistoria.
Janga la virusi vya corona limeuathiri Umoja wa Ulaya pakubwa. Raia wake 135,000 wamefariki dunia na uchumi wake unakadiriwa kunywea kwa asilimia 8.3 mwaka huu.