Umoja wa Ulaya haujafikia makubaliano ya pasipoti ya chanjo
19 Mei 2021Viongozi wa Umoja wa Ulaya hapo jana wameshindwa kuafikiana kuhusu kuanza kwa mpango wa pasipoti ya chanjo,Wazalishaji wa chanjo ya Covid-19 India wasitisha mpango wa kusaidia chanjo hiyo kwa matoafa yenye uhitaji na Sudan yapiga marufuku wasafiri kutoka India.
Ureno ambayo inashikilia uraisi wa Umoja wa Ulaya imesema washiriki kutoka Bunge la Ulaya, Halmashauri Kuu ya Umoja ya Ulaya na wajumbe kutoka katika mataifa wanachama wanatarajiwa kurejea tena na mazungumzo hayo kesho Alhamis. Cheti cha kidijitali kinatajwa kutoa uwezekano wa kuruhusu watu kusafiri ndani ya Umoja wa Ulaya kabla ya Juni, hata kama janga la virusi vya corona litaendelea na wasiwasi juu ya aina mpya ya virusi utasalia kuwa wa kiwango cha juu.
Katika vizuizi vya mipaka msafiri atapaswa kuonesha cheti cha hali ya afya yake.
Nyaraka hiyo itapaswa kuonesha kama msafiri amepima virusi na yupo salama au tayari amechanjwa kinga ya virusi hivyo.
Wazalishaji wa chanjo ya virusi vya corona nchini India wameonesha ule mpango wao wa kupeleka dozi za chanjo katika mataifa masikini utasitishwa hadi mwishoni mwa mwaka.
Hatua hiyo ya kucheleweshwa kwa usafirishaji wa chanjo kunatajwa kuwa piga kubwa kwa mpango wa usambazaji chanjo kwa mataifa masiki Covax unaoratibiwa na Shirika la Afya UlimwenguniWHO. Kupitia mpango wazalishaji hao walitarajiwa kutoa dozi milioni 110. India kwa sasa inashika nafasi ya pili kwa maambukizi duniani baada ya Marekani ikitajwa kuwa na watu waliombukizwa zaidi ya milioni 25.
Viwango vya maambukizi vimeongezeka Ujerumani.
Nchini Ujerumani taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza, Robert Koch leo inaonesha kiwango cha maambukizi kimeongezeka kwa rekodi za maambukizi mapya 11,040 na hivyo kufanya idadi juma kufikia watu milioni 3, 614,095. Na vifo vipya 284 na kufanya jumla ya watu 86,665.
Serikali ya Sudan imezuia wasafiri kutoka India kuingia nchini humo na kuweka masharti mapya ya kukabiliana na janga la virusi vya corona yakiwemo ya kufunga shule, katika kipindi hiki amabcho kiwango cha maambukizi kinaongezeka.
Taarifa ya baraza la uongozi la taifa hilo imesema itawazuia wasafiri wote wanaingia moja kwa moja kutoka India au hata waliopitia mataifa mengine katika kipindi cha siku 14. Lakini wasafiri kutoka Misri na Ethiopia watapimwa baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege.
Kwa rekodi za Mei 16, Sudan ina maambukizi 34,707 na vifo 1,116. Serikali inahofia idadi ya maambukizi inaweza kupindukia watu 100,000 katika juma la kwanza au la pili la mwezi Juni endapo hakujachukuliwa hatua madhubuti.
Vyanzo: DPA/RTR/AFP