Umoja wa Ulaya huenda ukarefusha Brexit
23 Oktoba 2019Swali ni je wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya watakubali kuipatia Uingereza muda zaidi kujitoa kutoka kundi hilo la mataifa kupindukia muda iliojiwekea wa mwisho wa tarehe 31 Oktoba, na kama watakubali, uchelewesho huo utakuwa vipi?
Rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk amesema atayashauri mataifa wanachama wengine 27 kukubali ombi la kuahirisha kutoka katika serikali ya Uingereza, ambalo Johnsonn amelazimishwa kuwasilisha siku ya Jumamosi chini ya sheria ya Uingereza baada ya kushindwa kupata uungwaji mkono wa wabunge kwa ajili ya makubaliano yake mapya.
Hata hivyo , mapema jana Jumanne wabunge walitoa idhinisho kwa sheria inayoidhinisha makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na Umoja wa Ulaya wiki iliyopita, na kisha kuzuwia muongozo wa waziri mkuu wa utaratibu wa kupitisha makubaliano hayo kabla ya muda wa tarehe 31 , Oktoba wa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya. Boris Johnson alisema.
"Sitakubali kabisa kuruhusu miezi zaidi kuhusu hili. Iwapo bunge litakataa kuruhusu Brexit kutokea na badala yake litaamua kuchelewesha hadi Januari ama huenda zaidi, katika hali hiyo serikali haitaweza kuendelea hivi. Mswada utabidi uondolewa na kulazimika kuitisha uchaguzi mkuu."
Ujerumani yatoa ishara
Hata hivyo Ujerumani imeonesha kuwa itakuwa tayari kutoa uchelewesho wa muda mfupi kwa ajili ya Brexit iwapo itakuwa ni sababu sahihi ya kisiasa, amesema hayo waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas katika mahojiano leo. Tunahitaji kufahamu, nini sababu ya hatua hii ? Maas alikiambia kituo cha televisheni cha binafsi nchini Ujerumani n-tv, na kuongeza iwapo itakuwa juu ya kurudisha tarehe nyuma kwa wiki mbili ama tatu kuruhusu wabunge mjini London kutekeleza hatua za kuidhinisha mswada wa kujitoa katika njia iliyo sahihi, nafikiri hii haitakuwa tatizo.
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson jana alisema uamuzi ni wa Umoja wa Ulaya iwapo wanataka kuchelewesha Brexit na kwa muda gani.
Johnson amewaambia wabunge jana baada ya kupiga kura kukataa idhinisho la moja kwa moja la Brexit, kwamba sera ya serikali bado ni kutochelewesha, na kwamba Uingereza inapaswa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya Oktoba 31. Hicho ndio nitawaambia Umoja wa Ulaya, amesema Boris Johnson.