1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Italy

EU kuisadia Italia kukabiliana na wimbi la wakimbizi

Sylvia Mwehozi
18 Septemba 2023

Umoja wa Ulaya umewasilisha mpango wa dharura wa kuisaidia Italia kuweza kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi ambao mnamo wiki iliyopita walivunja rekodi baada ya kuwasili kwa wingi katika kisiwa chake cha Lampedusa.

Italia | Ursula von der Leyen -Lampedusa
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akiwa kisiwani LampedusaPicha: Cecilia Fabiano/LaPresse/AP/dpa/picture alliance

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen siku ya Jumapili alikitembelea kisiwa cha Lampedusa ambacho kinapambana na ongezeko kubwa la wahamiaji wanaowasili na kuahidi mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuisaidia Italia kushughulikia hali hiyo.

Von der Leyen aliongozana na waziri mkuu wa Italia Giorgia Melonihuku gari iliyokuwa imewabeba kuelekea katika kituo cha kuwapokea wakimbizi kisiwani Lampedusa ikizuiwa kwa muda na wakaazi waliokuwa wakipinga mzigo unaokikabili kisiwa hicho. Kufuatia ziara yake hiyo, von der Leyen, ambaye anatarajiwa kuwania muhula wa pili, aliwasilisha mpango wa utekelezaji wenye vipengele 10 ili kuipunguzia Italia shinikizo la kuwapokea wakimbizi wanaowasili kwa maboti kutokea Afrika ya Kaskazini. Von der Leyen alisema chini ya mipango hiyo, "Umoja wa Ulaya utahakikisha nani anaingia Ulaya na chini ya mazingira gani na sio wasafirishaji haramu wa binadamu."

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na waziri mkuu wa Italia Giorgia MeloniPicha: YARA NARDI/REUTERS

"Nimekuja hapa kusema kwamba uhamiaji ni changamoto ya Ulaya na inahitaji jawabu na suluhisho la Ulaya. Ni hatua thabiti ambazo zitaleta mabadiliko. Ni kupitia mshikamano na umoja ambapo tunaweza kufanikisha hilo, na Umoja wa Ulaya utakuwa nanyi," aliongeza von der Leyen.

Mpango huo unajumuisha kuliwezesha shirika la ulinzi wa mipaka la Umoja wa Ulaya Frontex pamoja na lile la kuwapokea waomba hifadhi EUA, kusajili wahamiaji wanaowasili Italia na kuwarejesha nyumbani wale wasiokidhi vigezo. Takribani wahamiaji 126,000 wamewasili Italia tangu mwaka huu unaze, ikiwa ni karibu mara mbili ya idadi kama hiyo kwa takwimu za mwaka jana.

Naye waziri mkuu Meloni alisema suala la wahamiaji na la Umoja wa Ulaya vilevile; "Lakini nataka kusema kwamba sichukulii hii kama ishara ya mshikamano wa Ulaya kuelekea Italia, naiona kama ishara ya uwajibikaji kwa Ulaya yenyewe. Kwa sababu hii sio tu mipaka ya Italia, lakini pia ni mipaka ya Ulaya."

Wakimbizi wakiwasili kisiwani Lampedusa Picha: Cecilia Fabiano/AP Photo/picture alliance

Hatua hizo pia zitahakikisha wahamiaji wanachukuliwa alama za vidole na kufanyiwa mahojiano ili waweze kukabidhiwa kwa mamlaka stahiki. Umoja wa Ulaya pia utaongeza msaada kwa ajili ya kuwasafirisha waomba hifadhi kutoka Italia hadi nchi nyingine wanachama wa Umoja huo, chini ya mpango wa hiari wa kugawana wahamiaji, hususan wanawake na watoto wadogo wasioandamana na wakubwa.Kauli ya Meloni kuhusu wimbi la wakimbizi: Waziri Mkuu wa Italia aapa hatua kali kuzuia wahamiaji

Lakini mpango huo mara kadhaa umepingwa na baadhi ya nchi wanachama zikiongozwa na  Poland na Hungary. Wiki hii kwa mfano Ujerumani ilitangaza kwamba imesitisha kuwapokea wanaowasili kutokea Italia chini ya mpango huo ikisema kwamba Roma inashindwa kutimiza wajibu wake chini ya sheria za Umoja wa Ulaya.

Kisiwa cha Lampedusa kimeshuhudia ongezeko la wahamiaji wanaowasili kwa maboti, huku zaidi ya wahamiaji 7,000 wakiorodheshwa kuwasili wiki hii, idadi ambayo inapindukia wakaazi wa kisiwa hicho.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW