Umoja wa Ulaya kujadili vikwazo vipya kwa Urusi na washirika
10 Mei 2023Mazungumzo kati ya wajumbe wa Umoja wa Ulaya yameanza asubuhi hii mjini Brussels, Ubelgiji, kujadili pendekezo la vikwazo vipya dhidi ya Urusi na kuruhusu vizuizi vya usafirishaji kwa nchi ya tatu kwa kukiuka vikwazo vya biashara vilivyopo.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wanaotaka Urusi ichukuliwe hatua zaidi wameelezea kusikitishwa na mpango huo wakisema hauendi mbali sana, lakini wengine wanahofia unaweza kuharibu uhusiano wao wa kimataifa.
Urusi yadungua ndege zisizo na rubani
Wakati mkutano huo ukiendelea, gavana wa jimbo la Urusi la Voronezh, Alexander Gusev amesema kwamba ndege mbili zisizo na rubani zilijaribu kulishambulia eneo la jeshi katika jimbo hilo, lakini hazikufanikiwa.
Gusev ameandika katika mtandao wa Telegram kwamba vikosi vya ulinzi vya Urusi vilifanikiwa kuzidungua ndege hizo katika mkoa wa Kursk unaopakana na Ukraine. Amesema kwamba mabaki ya ndege hizo zilizoharibiwa, yaliangukia katika bomba la gesi na nyumba moja na kuziharibu vibaya.
Nalo jeshi la Ukraine limesema kuwa vikosi vyake vimezuia mashambulizi 46 katika kipindi cha saa 24, kwenye eneo la mashariki la Donetsk, ikiwemo mji wa Bakhmut. Kwa mujibu wa jeshi hilo, pia limefanya mashambulizi manane dhidi ya vituo vya kijeshi vya Urusi, pamoja na mashambulizi mawili katika mfumo wa kuzuia makombora.
Wakati huo huo, mkuu wa vikosi vya Ujerumani, Carten Breuer amesema vikosi vya Ukraine vinazidi kujiandaa kwa mashambulizi dhidi ya vikosi vamizi vya Urusi. Akizungumza leo na shirika la habari la Ujerumani, DPA baada ya kurejea kutoka Ukraine, Breuer amesema alifahamishwa jinsi mapigano yanavyofanyika katika maeneo ya mapambano.
Amesema ni wazi kwake majadiliano yote ya kupanga mashambulizi ya Ukraine, yanaendelea. Katika ziara yake hiyo, Brauer afisa wa ngazi ya juu kabisa katika jeshi la Ujerumani, alikutana na mkuu wa majeshi wa Ukraine, Valery Zaluzhny na Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Olexiy Resnikov.
Uingereza na Marekani kuendelea kuisaidia Ukraine
Hayo yanajiri wakati ambapo Uingereza na Marekani zimesema zitaendelea kuisaidia Ukraine hadi itakapofanikiwa katika mzozo huo. Katika mkutano wa pamoja na waandishi habari, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, James Cleverly amesema nchi hizo mbili zitaendelea kuiunga mkono Ukraine na ulimwengu haupaswi kuikumbusha Urusi kila wiki kuacha kutumia njaa ya watu kama silaha dhidi ya vita vya Ukraine
"Na tunahitaji kuendelea kuwasaidia, bila kujali kama mashambulizi yanayokuja yatafanikiwa, unajua faida kubwa ya kushinda katika vita. Kwa sababu mzozo huu hautaisha hadi utakapotatuliwa ipasavyo," alifafanua Cleverly.
Ama kwa upande mwingine Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema mazungumzo ya amani ya kuumaliza mzozo wa Ukraine hayawezekani kufanyika kwa sasa. Guterres amesema ana matumaini kuwa siku zinazokuja watafanikiwa kuwaleta pamoja Urusi na Ukraine kwenye meza ya mazungumzo.
(AFP, DPA, Reueters)