Umoja wa Ulaya kulipa msaada kwa serikali mpya ya Palestina
18 Juni 2007Umoja wa Ulaya unauunga mkono upande wa rais wa Wapalestina Mahmud Abbbas na chama chake cha Fatah ambacho kimeunda serikali mpya ya Palestina lakini kinadhibiti eneo la Magharibi mwa mto Jordan tu.
Kabla ya mazungumzo juu ya Palestina kuanza, waziri wa nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier alitathmini hali ilivyo katika maeneo ya Wapalestina: “Katika siku za nyuma tuliona vile hali ilivyozidi kuwa ni kali. Ni wazi kwamba kuongezeka kwa matumizi ya nguvu kumesababishwa na wanamgambo wa Hamas.”
Sasa inabidi kufanya kila kinachowezekana kumuunga mkono waziri mkuu mpya Salam Fajjad, alisema mwakilishi maalum kwa masuala ya nje wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana. Hatua moja inayozingatiwa ni kulainisha vikwazo vya kifedha dhidi ya Wapalestina. Solana alisema, sehemu fulani ndogo ya ofisi za mamlaka ya Wapalestina katika eneo la Magharibi mwa mto Jordan zitapewa msaada wa kifedha moja kwa moja. Msaada unaopewa kwa eneo la Gaza utatumwa kupitia mashirika ya misaada ya kimataifa.
Javier Solana alisema: “Kiwango fulani cha fedha hizo zitalipwa moja kwa moja. Vipi tutakavyotuma fehda kwenye eneo la Gaza, bado itabidi kutafute njia. Kwa hivyo lazima tuzungume na waziri mkuu Fajjad. Tumeshazungumza jana usiku, wakati huo hakujua la kufanya. Lakini ni muhimu sana, apange bajeti ili kuwasaidia wakaazi wa eneo la Magharibi mwa Jordan na katika ukanda wa Gaza.”
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya leo wamemualika pia waziri mwenzao wa Israel, Zipi Livni. Mjini Luxemburg, Bi Livni alisema kuwa Israel iko tayari kushirikiana na wale wanaotambua taifa la Israel. Ikiwa serikali mpya ya Palestina itaitambua Israel, serikali ya Livni itakubali kurudisha malipo ya kodi kwa Wapalestina. Hadi sasa, Israel imezuia kulipa Dola Millioni 600 malipo ya forodha na kodi kwa Wapalestina.
Kamisha wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Bibi Benita Ferrero-Waldner alisisitza kuwa kabla ya kuanzisha upya mahusiano rasmi na serikali ya Palestina itabidi kuwepo uwazi na kupatikana na vifaa vya kuchunguza matumizi ya fedha. Alisema:
“Ikiwa tunalipa msaada moja kwa moja, itabidi tuweze kusimamia matumizi yake. Kwani, mimi ninabeba jukumu kwa matumizi ya fedha raia wa Ulaya walilipa kama kodi. Na bila shaka, serikali ya dharura bado haiko tayari.”
Kwa muda wa miezi 15 sasa, Umoja wa Ulaya unatuma msaada wa kifedha kwa hospitali au katika shule bila ya kuzingatia serikali ya Wapalestina chini ya chama cha Hamas. Vikwazo hivi vya kifedha vilitumika pia dhidi ya serikali ya muungano kati ya Hamas na Fatah.