Umoja wa Ulaya kuongeza misaada yake kwa Niger
27 Julai 2005Nchi za Umoja wa Ulaya zinataka kuongeza jitihada zao kuwasaidia watu wanaokumbwa na tatizo la njaa nchini Niger. Baada ya kurudi kutoka nchini humo, wajumbe wa Kamati ya Umoja wa Ulaya walitoa taarifa kwamba hali nchini Niger ni mbaya, lakini bado inaweza kubadilishwa kwa kutoa misaada. Stefan Steffenberg ambaye ni mjumbe wa shirika la misaada la Umoja wa Ulaya, anaeleza: „Sasa hali inazidi kuwa mbaya. Kwa hivyo tunaongeza jitihada zetu. Na hii inahusu kamati ya Umoja wa Ulaya, nchi fulani zenyewe kama Uingereza pamoja na Marekani.“
Stefan Steffenberg aliendelea kusema kwamba Umoja wa Ulaja utaungana na mashirika ya misaada kuanzisha vituo vya kuwagawia watu vyakula, ili kuwasaida watu wengi katika muda mfupi. Kutokana na tatizo la ukame pamoja na janga la nzige lililotokea mwaka uliopita, mifumo ya kienyeji ya kupeleka vyakula iliharibika kabisa. Idadi ya watu wanaokumbwa na njaa nchini Niger inakadiriwa kati ya millioni 2.5 na millioni 3.6.
Tayari mwezi wa Novemba mwaka jana, Umoja wa Mataifa uliomba dola millioni 30 kupambana na tatizo la njaa katika nchi za eneo la Sahel lenye ukame. Lakini mpaka sasa ulipewa Dola millioni 10 tu. Vile vile ombi la Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa la kupatiwa dola millioni 16 limejibiwa kwa dola millioni 6 tu mpaka sasa. Kutokana na hali hii, Shirika la kimataifa la kutoa misaada, „Oxfam“, lilidai kwamba Umoja wa Mataifa uanzishe mfuko maalum wa dola billioni moja kwa ajili ya kuzuia majanga kama hili la Niger.
Kulingana na mkurugenzi wa shirika hilo la Oxfam, Bwana Phil Bloomer, mfuko kama huo ungeweza kuhakikisha kwamba nchi kama Niger ikihitaji misaada itaipata moja kwa moja bila ya kusubiri nchi fadhili kutoa pesa. Bwana Bloomer alisema kuwa ni jambo la kukasirisha sana kwamba dunia yote inasubiri mpaka watoto wanakufa kutokana na njaa kabla ya kuwasaidia. Shirika la Oxfam pia limesema bei za kuzuia janga la njaa lililotabiriwa ingekuwa dola moja tu kwa kila mtu anayehusika, badala ya dola 80 zinazohitajika kwa kumwokoa mtu mmoja na kufa.
Wakati huo huo wajumbe wa Umoja wa Ulaya walizipinga lawama zinazosema kwamba nchi za Ulaya zilichelewa kulijibu onyo la janga la njaa nchini Niger. Walisema Umoja wa Ulaya ulikuwa na mpango ya kutoa Euro zaidi ya millioni mia tatu kwa ajili ya kujenga mfumo wa kujitegemea. Stefan Steffenberg alieleza:
“Siyo kama tumeshtukizwa kabisa na hali ya Niger. Haijatokei tu wiki iliyopita, kwa sababu tangu wakati huo tumeona picha kwenye taarifa za habari ndani ya televisheni. Wajumbe wetu wameiangalia hali ya Niger kila siku na wakachunguza vipi tunaweza kutafuta washirika wengine kuzizuia shida zinazoweza kutokea.“
Sababu kuu ya hali kuwa mbaya zaidi ni ukame katika eneo hili la Afrika Magharibi. Zaidi ni kwamba nchi ya Niger haina muundo mbinu unaofaa kuwagawia watu misaada ya haraka.
Sasa Umoja wa Ulaya utatoa Dola millioni 5.5 kununulia vyakula na maji kwa watu wa Niger. Lakini pia umesisitiza kwamba nchi nyingine za Afrika zinakumbwa na tatizo la njaa kutokana na ukame na nzige. Kwa hivyo Umoja wa Ulaya utazipa Mali Dola millioni 2,5 na Dola millioni 10 kwa Ethiopia na Kenya kwa ajili ya kununulia vyakula, mbegu na mifugo. Katika nchi hizi tatu mamia kwa maelfu ya watu wanakumbwa na hali mbaya, walisema wajumbe wa Umoja wa Ulaya.