Umoja wa Ulaya kusaidia kulinda mipaka ya Libya
31 Januari 2013Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Bi Catherine Ashton, ameeleza kwamba hatua ya kuongeza uwezo wa Libya kulinda mipaka yake ni ya muhimu, si kwa nchi hiyo tu bali kwa eneo zima. Tangu kuangushwa madarakani kwa Muamar Gaddafi mwaka 2011, Libya imekumbwa na changamoto kulinda mipaka yake yenye ulinzi finyu. Wataalamu wanaamini kwamba silaha kutoka Libya zimekuwa zikivushwa na kupelekwa katika nchi jirani kama Mali, ambapo zinatumika kwenye mapigano.
Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wameeleza kwamba utawala wa Libya umeshindwa kudhibiti hasa mpaka wake wa kusini unaoitenga nchi hiyo na Algeria, Niger, Chad na Sudan. Inaelezwa kwamba watu wenye kubeba silaha nzito nzito huuvuka mpaka wa Libya na kupitisha silaha na madawa ya kulevya kimagendo. Wataalamu wa Umoja wa Ulaya wamelenga kutoa mafunzo kwa maafisa wa usalama wanaolinda mipaka ya Libya ili kuimarisha usalama. Wataalamu hao watapelekwa Libya kwa kipindi cha miaka miwili kwanza na baadaye muda wao unaweza kuongezwa kwa mwaka mmoja.
Uingereza yaahidi kuisaidia Libya
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amefanya ziara ya kushtukiza katika mji mkuu wa Libya, Tripoli. Ziara ya Cameron inakuja siku chache tu baada ya Uingereza kutoa angalizo juu ya tishio la mashambulizi kwa ubalozi wa nchi yake uliopo Tripoli. Ofisi ya waziri mkuu huyo ilitoa taarifa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, inayoeleza kwamba Cameron anakwenda Libya kujadili namna ambavyo Uingereza inaweza kusaidia katika kujenga Libya yenye nguvu, ustawi na demokrasia.
Baada ya kuwasili, Cameron na waziri wa mambo ya ndani wa Libya Ashur Shwayel walikitembelea chuo kimoja cha polisi ambapo ilifanyika hafla ya kuwapandisha cheo maofisa wa polisi. Cameron yuko njiani kuelekea Liberia ambapo atahudhuria mkutano wa kiamataifa kuhusu maendeleo.
Katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, ilizungumziwa pia hali nchini Mali. Mawaziri hao wamewataka wanajeshi wa nchi za Afrika kuchukua nafasi ya wanajeshi wa Ufaransa haraka iwezekanavyo. Waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji, Didier Reynerds, amesema kwamba anatarajia kuwa operesheni inayoendelea Mali itakuwa ya kimataifa na itakayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na majeshi ya nchi za Kiafrika.
Nchini Mali kwenyewe msemaji mmoja wa jeshi ameeleza kwamba bomu la kutegwa ardhini limewaua wanajeshi wanne na kujeruhi wengine watano baada ya gari walilokuwa wakisafiria kufyatua bomu hilo.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef