1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kutathmini upya uhusiano wake na Tanzania

Daniel Gakuba
16 Novemba 2018

Umoja wa Ulaya umesema unazitafakari sera zake kuhusu Tanzania, na utafanya mjadala na nchi hiyo baada ya kukamilika tathmini hiyo. Serikali ya nchi hiyo inakosolewa kukanyaga haki za binadamu na kuhujumu demokrasia.

Federica Mogherini Hohe Vertreterin der EU für Außen- und Sicherheitspolitik
Federica Mogherini, mkuu wa sera za nje wa Umoja wa UlayaPicha: Getty Images/AFP/J. Thys

Tangazo lililotolewa jana na mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya Federica Mogherini, limesema nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinatiwa wasiwasi na hali ya hivi sasa kisiasa nchini Tanzania, ikiwemo kuzuiwa kwa uhuru wa vyombo vya habari na shughuli za vyama vya kisiasa, na vitisho dhidi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Hatua hii ya Umoja wa Ulaya inafuatia uamuzi wa Denmark, nchi ya pili kwa kuipatia msaada mkubwa Tanzania, kusitisha kiasi cha dola milioni 10 za kimarekani kwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Benki ya dunia pia imesimamisha msaada wa dola milioni 300, ikilalamikia sera ya Tanzania ya kuwafukuza shuleni wasichana waliobeba mimba, na kuweka sheria inayoadhibu kitendo cha kukosoa takwimu zinazochapishwa na serikali.

Sakata la kuwatimua wasichana wanaobeba mimba

Mkurugenzi wa kitengo cha Afrika katika Kituo cha kutetea haki ya uzazi, Evelyne Opondo, ameliambia shirika la Thompson Reuters Foundation, kwamba hatua hiyo ya Benki ya Dunia ni ya kijasiri, na kutaka pande nyingine zinazotoa msaada mkubwa wa kimaendeleo kwa Tanzania zifuate mfano huo.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli. Serikali yake inashutumiwa kukandamiza uhuru wa kujieleza na haki za binadamu.Picha: DW/S. Khamis

Opondo alisema tayari Tanzania inao wasichana wengi walionyimwa fursa ya kupata elimu na kujiendeleza kimaisha, wakilazimishwa kuzama katika mzunguko wa umasikini, na kusisitiza kwamba yale yanayohimizwa na Benki ya Dunia kwa Tanzania, yamo ndani ya uwezo wa serikali ya nchi hiyo.

Balozi aondoka chini ya shinikizo

Umoja wa Ulaya umesema shinikizo la serikali ya Tanzania lilimlazimisha balozi wake kuondoka nchini humo na kurejea mjini Brussels, ukisema hali hiyo inakwenda kinyume na uhusiano uliozoeleka baina ya pande hizo wa kujadiliana na kushauriana. Mapema mwezi huu wa Novemba, Umoja wa Ulaya ulimwita nyumbani balozi wake wa Tanzania, katika kupinga tangazo la kuanza kuwaandama mashoga.

Mwezi Juni mwaka Jana, Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli alitoa kauli ya kuunga mkono sheria ya kuwafukuza wasichana wanaobeba mimba wakiwa katika shule za serikali, ambayo ilitungwa mwaka 1961, akisema hali hiyo inakiuka maadili.

Watetezi wa haki za binadamu wanasema tangu kutolewa kauli hiyo ya Rais Magufuli, wasichana wanaobeba mimba wamekuwa wakikamatwa, huku wabakaji wakisamehewa, na wanatoa hoja kwamba wasichana wadogo wanapaswa kuchukuliwa kama wahanga, sio kama wahalifu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre,dpae

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW