1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya

Abdu Said Mtullya11 Desemba 2009

Nchi zinazoendelea kupatiwa bilioni 7.2 na Umoja wa Ulaya katika juhudi za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Sweden Fredrik Reinfeldt kwenye mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.Picha: AP

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameahidi kutoa Euro bilioni 2.4 kila mwaka kwa nchi zinazoendelea katika muda wa miaka mitatu ijayo.

Viongozi wa nchi na serikali wa Umoja huo wametoa ahadi hiyo baada ya mkutano wao wa siku mbili mjini Brussels.

Lengo la viongozi hao kutoa ahadi ya fedha ni kuzitaka nchi zinazoendelea ziziunge mkono kwenye mkutano unaojadili mabadiliko ya hali ya hewa unaofanyika mjini Copenhagen-Denmark.

Nchi za Umoja wa Ulaya zitatenga jumla ya Euro bilioni 7.2 ili kuzisaidia nchi masikini katika juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa .

Ujerumani peke yake itachangia Euro bilioni 1.2

Ndiyo kusema katika kipindi cha miaka mitatu ijayo Ujerumani itatoa Euro milioni 420 kila mwaka kwa ajili ya nchi zinazoendelea.

Akifafanua juu ya ahadi ya nchi za Umoja wa Ulaya waziri mkuu wa Sweden Fredrik Reinfeldt ambaye sasa anauongoza Umoja huo kwa niaba ya nchi yake alisema mjini Brussels leo kwamba fedha hizo

ni mchango wa haraka kutoka nchi za Ulaya kwa ajili ya kuzisaidia nchi zinazoendelea ili ziweze kukabiliana na madhara yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Waziri mkuu Reinfeldt pia amesema nchi za Ulaya zinatoa pendekezo la kupunguza gesi chafu kwa asilimia 30 hadi kufikia mwaka 2020 katika msingi wa viwango vya mwaka 1990, ikiwa nchi nyingine tajiri za viwanda nazo zitakuwa tayari kuchukua hatua kama hiyo.

Mkuu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia hali ya hewa Yvo de Boer amesema umauzi wa nchi za Umoja wa Ulaya kutenga fedha hizo kwa ajili ya nchi zinazoendelea ni mchango mkubwa katika juhudi za kuyafanikisha mazungumzo kwenye mkutano wa mjini Copenhagen.

Lakini China imesema ahadi za muda mfupi siyo jawabu la mabadiliko ya hali ya hewa.

Mwandishi/Mtullya/AFPE/ZA

Mhariri/Abdul-Rahman


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW