1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuwaidhinisha viongozi wakuu wa taasisi hiyo

27 Juni 2024

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wako tayari kuwaidhinisha Von der Leyen, António Costa na Kaja Kallas kama viongozi wakuu wa taasisi hiyo inayoyajumuisha mataifa 27 kwa miaka ijayo. Sera ya biashara ndio jukumu lao kubwa

Ursula Von De Leyen
Ursula Von De Leyen atapendekezwa kwa muhula wa pili kama rais wa Kamisheni ya UlayaPicha: EPA/Denis Balibouse

   
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wako tayari kuwaidhinisha Ursula von der Leyen, António Costa na Kaja Kallas kama viongozi wakuu wa taasisi hiyo inayoyajumuisha mataifa 27 kwa miaka ijayo, jukumu lao kubwa likiwa ni kutengeneza sera kubwa zaidi ya biashara duniani.

Baada ya majadiliano marefu kati ya makundi matatu makubwa katika bunge la Ulaya, hatimaye makubaliano yalifikiwa mapema wiki hii ambapo Ursula von der Leyen, António Costa na Kaja Kallas wanatarajiwa kupitishwa katika mkutano wa kilele wa siku mbili unaofanyika mjini Brussels, licha ya ukosoaji kutoka kwa wanasiasa wa mrengo wa kulia.

Soma zaidi. Brussels yaimarisha usalama kuelekea mkutano wa kilele wa EU

Chini ya makubaliano yaliyofikiwa na wasuluhishi kutoka kwa wahafidhina, wafuasi wa mrengo wa kati wa Kisoshalisti na waliberali ni kwamba Mjerumani von der Leyen atapendekezwa kwa muhula wa pili kama rais wa Kamisheni ya Ulaya, na Kosta aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Ureno atapendekezwa kuchukuwa nafasi ya Rais wa Baraza la Ulaya iliyokuwa chini ya Charles Michel.

Kwa upande wake Kallas,  Waziri Mkuu wa Estonia anayejulikana kwa msimamo wake linapokuja suala la Urusi, anapendekezwa kuwa mwanadiplomasia mkuu wa Umoja huo kuchukua nafasi ya Josep Borrell.

Kaja Kallas, Waziri Mkuu wa EstoniaPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Soma zaidi. Urusi yafungia baadhi ya vyombo vya habari vya Ulaya

Uteuzi wa Kosta utaamuliwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya huku von der Leyen na Kallas wao watahitaji kuidhinishwa na wabunge.

Meloni: Siungi mkono kuchaguliwa kwa viongozi hao watatu

Uchaguzi wa Bunge la Ulaya uliofanyika Juni 6 hadi 9 ulishuhudia uungwaji mkono mkubwa wa vyama vya mrengo mkali wa kulia katika mataifa ya Ufaransa na Ujerumani, ingawa ushindi huo haukuwapa wingi wa viti mbele ya vyama hivyo vitatu vinavyolitawala Bunge la Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Italia, Georgia Meloni amaeukosoa uamuzi wa kuwachaguwa viongozi hao watatu akisema sio matakwa ya raia wa Umoja wa Ulaya.

Giorgia Meloni, Waziri Mkuu wa ItaliaPicha: Domenico Stinellis/AP Photo/picture alliance

"Bila shaka, wapo pia wanaoamini kuwa wananchi hawajakomaa vya kutosha kufanya maamuzi fulani na kwamba watu wachache wanaweza kufanya maamuzi. Lakini mimi sio muumini wa maoni kama hayo. Nimepingana na kanuni kama hizi nchini Italia. Nina nia ya kupingana nazo hapa Ulaya pia. Tuna hakika kwamba wananchi wako sahihi siku zote na kwamba ni wajibu wa yeyote mwenye nafasi ya kuwajibika kufuata matakwa yanayotoka kwa wananchi." Giorgia Meloni.

Soma zaidi. Ukraine inajiandaa na majadiliano ya kujiunga na EU

Kwenye mkutano huo wa siku mbili, viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesaini makubaliano ya usalama na Ukraine, ambayo yanaufanya kile upande kuwa na wajibu wa kuusaidia mwengine wakati usalama wake unapohatarishwa.

Rais Volodymyr Zelensky ambaye amehudhuruia mkutano huo amewashukuru viongozi hao wa Ulaya na kuendelea kuwaasa waipe nchi yake msaada zaidi.

Vyanzo: AP/ Reuters


 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW