Umoja wa Ulaya na Canada zasaini makubaliano ya CETA
30 Oktoba 2016Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na viongozi wa Umoja wa Ulaya Jumapili (30.10.2016) hatimae wamesaini makubaliano ya kihistoria ya biashara yaliyochukuwa miaka saba kutayarishwa na ambayo yalikuwa nusura yasambaratishwe na mkoa mmoja mdogo wa Ubelgiji.
Hafla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo mjini Brussels iliahirishwa kutoka Alhamisi baada ya mkoa wenye wakaazi milioni 3.5 tu wanaozungumza Kifaransa wa Wallonia awali kutumia kura yake ya turufu kupinga makubaliano hayo yenye taathira kwa zaidi ya watu milioni 500 wa Ulaya na wananchi milioni 35 wa Canada.
Shangwe na vifijo viliripuka wakati Trudeau akisaini makubaliano hayo pamoja na Rais wa Barazan la Umoja wa Ulaya Donald Tusk, Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean -Calude Juncker na Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico ambaye nchi yake inashikilia urais wa kupokezana wa umoja huo.
Awali waandamanaji walipenya safu ya polisi wa kuzuwia fujo na kumwaga rangi nyekundu kwa makao makuu ya Umoja wa Ulaya huku wanaharakati wakicheza ngoma na kutowa kauli mbiu zenye kupinga makubaliano hayo Kabambe ya Kiuchumi na Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Canada.
Kuanza kwa mkutano huo wa kilele kumezidi kucheleweshwa wakati ndege ya Trudeu ilipolazimika kurudi nyumbani kwa muda kutokana na matatizo ya kufundi.
Ushuru kuondolewa
Makubaliano hayo ya CETA yanaondowa ushuru wa forodha kati ya pande hizo mbili na kuliunganisha soko la pamoja la Ulaya na nchi yenye kushikilia nafasi ya kumi kwa kuwa na uchumi mkubwa duniani.
Sakata hilo la Ubelgiji liliibuwa tahadhari kuhusu kuaminika kwa Umoja wa Ulaya kama mshirika wa kibiashara wakati huku ikiwa imezongwa na hatua ya kufadhaisha ya Uingereza kujitowa Umoja wa Ulaya,mzozo wa wahamiaji na kuibuka upya kwa Urusi.
Baada ya mazungumzo za miaka mingi makubaliano hayo yalikuwa nusura yasambaratike na Trudeu alikubali Ijumaa usiku kwenda Brussels baada ya Wallonia kukubali hatimae kujiunga na mikoa iliobakia ya Ubelgiji na nchi nyengine wanachama 27 za Umoja wa Ulaya kuidhinisha makubaliano hayo.
Nchi zote zilitakiwa ziuidhinishe
Mkataba huo ulikuwa ukitaka nchi zote za Umoja wa Ulaya ziuidhinishe na katika baadhi ya kesi kama vile Ubelgiji serikali za mikoa zilitakiwa pia kufanya hivyo na hiyo kutowa fursa kwa mkoa wa Wallonia kuwa na uwezo wa kura ya turufu.
Mkoa huo wa Wallonia ulihimili shinikizo kubwa kwa wiki mbili kutoka pande zote mbili hadi pale iliporidhiwa madai yake katika maslahi ya kilimo na hakikisho kwamba wawekezaji wa kimataifa hawatoweza kuzilamisha serikali kubadilisha sheria.
Wasi wasi wa kudhoofika kwa mkoa huo ulioendelea kiviwanda ulioko kusini mwa Ubelgiji unaonyesha wasi wasi wa jumla ulioko barani Ulaya kuhusu utandawazi halikadhalika hofu miongoni mwa wanaharakati kwamba makubaliano ya aina hiyo yanadhoofisha ulinzi kwa mlaji , jamii na mazingira.
Mwandishi Mohamed Dahman AFP
Mhariri Sekione Kitojo