1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya na hatua za kisheria dhidi ya Uingereza

Sylvia Mwehozi
1 Oktoba 2020

Umoja wa Ulaya umechukua hatua za kisheria dhidi ya Uingereza kuhusiana na mipango yake ya kupitisha sheria itakayokiuka baadhi ya vipengele vya makubaliano ya mchakato wa kujiondoa kwenye muungano huo.

Belgien Brüssel | Pressekonferenz Brexit | Ursula von der Leyen
Picha: Johanna Geron/AP Photo/picture-alliance

Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema wameamua kutuma barua rasmi kwa serikali ya Uingereza ikiwa ni hatua ya kwanza katika mchakato wa ukiukwaji. Sakata hilo la ukiukaji makubaliano ambalo linaweza kufikishwa mbele ya mahakama za Umoja wa Ulaya, halijazuia mazungumzo ya biashara ya baada ya Brexit, lakini linadhihirisha mvutano unaozidi kuongezeka baina ya pande hizo mbili kadri muda unavyoyoyoma. Von der Leyen amesema barua hiyo inaitaka Uingereza kutuma maelezo zaidi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja. Zaidi amesema kwamba; "Kama mjuavyo tuliwajulisha marafiki zetu wa Uingereza ili waondoe sehemu yenye shida katika rasimu ya muswada wa soko la ndani kufikia mwishoni mwa Septemba. Rasimu ya muswada huu kwa asili yake ni ukiukaji wa wajibu wa makubaliano yaliyofikiwa kwa nia njema. Ikiwa utaidhinishwa kama ulivyo utakuwa ni kinyume na itifaki ya Ireland na Ireland ya Kaskazini. Muda wa mwisho umemalizika jana na vifungu vyenye shida havijaondolewa."

Siku ya Jumanne wabunge wa Uingreza waliupitishwa muswadahuo wa kudhibiti soko la ndani kuanzia Januari mosi, wakati ambapo taifa hilo litakapokuwa linamaliza kipindi chake cha mpito cha baada ya Brexit na kuondoka katika soko la pamoja la Umoj wa Ulaya na muungano wa forodha.

Waziri Mkuu wa Uingereza Borris JohnsonPicha: picture-alliance/empics/House of Commons

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wana hofu kwamba ikiwa muswada huo utasainiwa kuwa sheria, utasababisha kuanzishwa tena kwa udhibiti mkali wa mipaka ya ardhini kati ya Ireland ya Kaskazini ambayo ni sehemu ya Uingereza na Jamhuri ya Ireland ambayo mwanachama wa Umoja wa Ulaya, na hivyo kudhoofisha utulivu ambao umeleta amani tangu makubaliano ya mwaka 1998. Kipengele cha tano cha makubaliano ya Brexit ndicho kinalalamikiwa na Umoja wa Ulaya ambacho kinaweka wazi kuwa pande zote lazima "zishikirikiane kwa nia njema" kutekeleza mpango huo.Soma EU, Uingereza zafanya kikao cha dharura

Muswada wa sheria hiyo unabatilisha baadhi ya vipengele vya makubaliano ya Brexit ambayo waziri mkuu Borris Johnson aliyasaini na Umoja wa Ulaya mwaka jana na hivyo kukiuka sheria za kimataifa. Hata hivyo serikali ya Johnson imeutetea muswada huo kuwa "ngao ya usalama" ikiwa mazungumzo ya biashara ya baada ya Brexit yatakwenda ndivyo sivyo na Umoja wa Ulaya kujaribu kuanzisha ushuru wa forodha mpakani baina ya Uingereza na Ireland ya Kaskazini.

Rasimu ya muswada huo bado itatakiwa kupitishwa na bunge la juu la Uingereza, ambako huenda ikakabiliwa na upinzani kwasababu ya kukiuka sheria za kimataifa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW