1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya na Marekani kuacha kwa muda kutozana ushuru

6 Machi 2021

Umoja wa Ulaya na Marekani zimekubaliana kuacha kwa muda kuzitoza ushuru wa thamani ya mamilioni ya dola bidhaa zinazoingia katika kila upande.

Deutschland Frankfurt Airbus A380 und Boeing 747
Picha: Boris Roessler/dpa/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden na rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen walifikia makubaliano hayo katika juhudi za kuujenga upya uhusiano baina ya Marekani na Ulaya uliovurugika katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Donald Trump. Baada ya mazungumzo ya simu Biden na von der Leyen walitambua umuhimu kwa pande mbili hizo kusimamisha kwa miezi minne, sera ya kutozana ushuru uliosababishwa na mgogoro kati ya mashirika yao ya kutengeneza ndege, shirika la Airbus la Ulaya na Boeing la Marekani. Mgororo huo umekuwa unaendelea kwa muda wa miaka 16.

Marekani imesimamisha toza ushuru ndege na bidhaa zingine zinazohusiana na ndege za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.  Vilevile haitatoza ushuru mvinyo na jamu kutoka Ufaransa na Ujerumani, na pia matunda ya mizeituni kutoka Uhispania. Bidhaa nyingine zilizomo kwenye orodha ya makubaliano hayo yaliyofikiwa siku ya Ijumaa ni pamoja na kahawa, pombe kali, jibini na nyama ya nguruwe kutoka Jumuiya ya Ulaya.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: EU Commission/AA/picture alliance

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen ameupongeza mwanzo huu mpya. Kutokana na makubaliano hayo, Rais Joe Biden amesema ataendelea kuurekebisha na kuutia nguvu uhusiano kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya. Kulingana nataarifa ya ikulu ya Marekani, Rais Biden amesema yeye na von der Leyen wamekubaliana kufanya kazi kwa pamoja kusuluhisha mizozo ya muda mrefu katika shirika la biashara ulimwenguni WTO.

Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Jonathan Ernst/REUTERS

Pande hizo mbili zimesema katika taarifa ya pamoja kwamba kusitisha tozo za ushuru kutaokoa kiasi cha dola bilioni 7.5 kutokana na bidhaa zinaoingia Marekani kutoka nchi za Umoja wa Ulaya na kiasi cha dola ilioni 4 kutokana na bidhaa za Marekani,zinazoagizwa kutoka Marekani hatua zilizotokana na mizozo hiyo ya muda mrefu ya mashirika ya ndege ya Airbus na Boeing iliyokuwepo kati ya pande mbili hizo katika Shirika la Biashara Duniani WTO. Viongozi hao wamesema hatua hiyo itapunguza mzigo kwa nchi hizo.

Mkuu wa maswala ya biashara wa Umoja wa Ulaya Valdis Dombrovskis pia ameusifu mwanzo huo mpya katika uhusiano wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na Marekani mshirika wake muhimu wa kibiashara. Amesema hatua hiyo ya kuondoa ushuru ni ushindi kwa pande zote mbili, wakati ambapo janga la corona limeathiri uchumi wa dunia.

Chanzo: https://p.dw.com/p/3qHbo