Umoja wa Ulaya na Uturuki magazetini
26 Februari 2013Ziara ya kansela Angela Merkel nchini Uturuki, ndoa za watu wa jinsia moja na kashfa ya nyama ya farasi kuenea mpaka katika mayai ya 'Bio' ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani hii leo. Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linaandika kuhusu ziara ya kansela Angela Merkel katika nchi inayopiga hodi tangu miaka minane iliyopita, kutaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, Uturuki.
Kansela Angela Merkel aliyeanza ziara yake mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Uturuki, hajenda kutoa nasaha, si leo - si kesho na si kwa yeyote kati ya viongozi wenzake. Hata hivyo Umoja wa Ulaya wanabidi watambue namna juhudi zao za kuania ushawishi katika eneo la mashariki la bahari ya kati, zitakavyokuwa. Kwa namna hiyo wanapaswa na wanabidi watoe masharti kwa mfano kuhusiana na kisiwa cha Cyprus na kuhusu pia haki za binaadam.Mtindo wa kuvuta wakati na kuchelewesha mambo unabidi ukome.
Gazeti la "Der Tagesspiegel" linahisi kila muda unapopita ndipo nayo Uturuki inapozidi kujiimarisha kwengineko. Gazeti linaendelea kuanadika. Waturuki kwa ghafla wanajikuta wakisifiwa. Pindi nchi hiyo ingekuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya,basi ingekuwa inashikilia hivi sasa nafasi ya sabaa ya mataifa yenye nguvu za kiuchumi katika umoja huo.Uturuki ni mwanachama wa kundi la mataifa 20-G-20 na ni mshirika muhimu wa Marekani. Kisiasa serikali ya Erdogan inaimarisha ushawishi wake barani Asia, Mashariki ya kati na barani Afrika.Kutoka muomba nasaha wa pembezoni mwa Ulaya,limegeuka hivi sasa kuwa dola linalojiamini na lenye kujivunia nguvu za kiuchumi. Wataalam wengi wa Umoja wa Ulaya wanaoshughulikia masuala ya Uturuki wanahisi kwa hivyo kimoja tu ndicho kinachoweza kuyanusuru mazungumzo ,nacho ni kama Brussels itatoa ahadi thabiti ya kuikubalia Uturuki uanachama.
Ndoa za watu wa jinsia moja
Gazeti la Thüringische Landeszeitung" linaandika kuhusu ndoa ya watu wa jinsia moja likisema imeingia pia midomoni, miezi sabaa kabla ya uchaguzi mkuu. Kwa maoni ya gazeti hilo, wapiga kura wanatambua zaidi ukweli wa mambo kuliko wanasiasa.Katika takriban familia nyingi tu kunakutikana angalao ndowa moja ya aina hiyo ambayo zamani wahusika walikuwa wakiweka siri ,wakijificha,au wakilazimika kukanusha.Na hasa katika maeneo ya mashambani,tangu miaka ya hivi karibuni jambo hilo limekuwa jambo la kawaida na ambalo wanasiasa wanapopita wakiwa ndani ya magari yao ya viyoo vya kiza hawalizingatii. Vyama ndugu vya CDU/CSU vingefanya la maana kuutambua ukweli wa maisha wa wapiga kura wao.Na ukweli huo wa maisha ni wa mchanganyiko mkubwa zaidi kuliko vile ambavyo baadhi wangependelea uwe.
Kashfa ya hadaa katika nyama ya farasi inaonyesha kuiathiri pia biashara ya mayai ya 'Bio' - yaani yale mayai ambayo yanatagwa na kuku wanaofungwa kwa njia za kiasili. Gazeti la Nordwest-Zeitung" linaandika la muhimu katika kashfa zote hizo ni kuhakikisha kwamba mwisho wahusika wanachukuliwa hatua zinazofaa.Ikiwa sekta husika haina uwezo,basi waachiwe wafanyabiashara.Mashirika ya kibiashara yanastahiki kudai uchunguzi wa kina na madhubuti ufanyike kuanzia mahala kuku wanakofugwa,idadi ya kuku hadi kufikia chakula wanachopewa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Josephat Charo