Umoja wa Ulaya umeiwekea vikwazo Myanmar
22 Februari 2022Mataifa wanachama ya umoja huo yamezuia mali na marufuku ya kusafiri kwa maafisa 22 na kadhalika kuzua makampuni manne, yakiwemo yanayomilikiwa na serikali pamoja na watu binafsi.
Miongoni mwa yaliwekewa vikwazo ni pamoja na yale yanayomilikiwa na serikali kama kampuni ya mafuta ya Myanmar lijulikanalo kama Myanma Oil na ya gesi, Enterprise (MOGE) yenye ubia wa pamoja. Vikwazo dhidi ya MOGE kunatokana na kampeni ya muda mrefu ya makundi ya haki za binaadamu ya Myanmar na kwengineko duniani, ambayo yalikuwa yanasema hatua hiyo inaweza kuuondolea utawala wa kijeshi kupata kipato cha kujiendesha kwake.
Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Myanmra asilimia 50 za mapato yake yatokanayo na fedha za kigeni yanatokana na rasilimali ya gesi, ambapo kampuni MOGE inakadiriwa kuliingizia taifa hilo kiasi cha dola bilioni 1.5 kwa mwaka 2021-2022. Katika duru za awali vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya dhidi ya Myanmar havikuigusa sekta ya gesi.
Wasiwasi wa hali kuendelea kuwa mbaya nchini Myanmar
Katika taarifa yake makao makuu ya Umoja wa Ulaya imesema ina wasiwasi mkubwa na hali ya kuendelea kwa machafuko nchini Myanmar na kuzuka na athari zake kikanda. Tangu kutokee mapinduzi ya kijeshi kwa mfululizo hali imeendelea kuzorota na kuwa mbaya zaidi.
John Sifton, ambae ni mkurugenzi wa utetezi wa kwa bara la Asia wa shirika la Human Rights Watch, ameonekana akipongeza uamuzi wa Umoja wa Ulaya kwa kusema vikwazo dhidi ya MOGE vilikuwa na umuhimu hasa ikizingatiwa jinsi mapato ya kampuni yalivyokuwa muhimu kwa wanajeshi.
Wimbi kubwa la maandamano ya amani nchini Myanmar lilitokana na mapinduzi ya Februari Mosi, 2021, dhidi ya kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia Aung San Suu Kyi. Kupingwa kwa jeshi kuliongezea baada ya ukandamizaji dhidi ya raia katika maandamano hayo.
Taifa hilo kwa sasa linakalibiliwa na uasi katika kiwango ambacho wataalam wanasema kama lipo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Takribani watu 1,500 wameuwawa kwa kuteswa au kuuwawa katika vurugu, ambapo mashambulizi mengi yametokea katika maeneo ya vijinini yakiwemo ya anga.
Hadi wakati huu Umoja wa Ulaya wenye mataifa 27, imeweka vikwazo kwa jumla ya watu 65 na taasisi 10, ambazo zinaweza kuwa mashirika, makampuni, vyama au benki.
Chanzo: AP