Umoja wa Ulaya umewawekea vikwazo maafisa sita wa Urusi
15 Oktoba 2020Umoja wa Ulaya na Uingereza zimetangaza leo vikwazo dhidi ya raia sita wa Urusi, kuhusu tukio la kupewa sumu kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalvy. Urusi ambayo imetupilia mbali vikwazo hivyo, inasema hatua ya umoja huo itahujumu uhusiano wake na Urusi. Zaidi na Saleh Mwanamilongo.
Vikwazo hivyo ni pamoja na kutowaruhusu maafisa hao kusafiri kwenye eneo la nchi za Umoja wa Ulaya, na kuzuiwa kwa mali zao. Kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo hivyo ni pamoja na Alexander Bortnikov, mkuu wa idara ya kiusalama ya Urusi na Sergei Kiriyenko, naibu kiongozi wa ofisi ya rais Putin.
''Vikwazo vimechukuliwa kwa kauli moja''
Waziri wa mamabo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas ambae nchi yake ndio inashikilia kiti cha kupokezana cha urais wa Umoja wa Ulaya, amesema ni msimamo wa wazi pekee na kuzingatia kanuni ambapo Umoja wa Ulaya utapiga hatua kuhusu mwelekeo wa heshima na Urusi.
''Urusi inatakiwa kuendelea kujieleza kuhusu shambulizi dhidi ya Alexei Navalny na matumizi ya sumu ya kemilaki ambayo imepigwa marufuku. Na tulisisitiza mara nyingi kwamba tabia kama hiyo haiwezi kuachwa hivi hivi bila kuchukuliwa hatua na hivyo vikwazo vimechukuliwa kwa kauli moja na kwa haraka na Umoja wa Ulaya.''
Vikwazo hivyo vinaihusu pia taasisi ya kitaifa ya utafiti wa kemikali na teknolojia. Uingereza imesema itatekeleza pia vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya maafisa hao wa Urusi na itaendelea kufanya hivyo baada ya kipindi cha mpito cha kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, Brexit, mwezi Desemba.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, Dominic Raab, ameishutumu Urusi kwa kuhusika na tukio hilo na kusema kwamba Uingereza itafanya kazi pamoja na washirika wake wa kimataifa, ili kuwawekea vikwazo maafisa wa Urusi na wengine waliohusika. Amesema matumizi yoyote ya silaha za kemikali ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa.
Vikwazo vya EU kuhujumu uhusiano na Urusi?
Haraka Urusi ilijibu kuhusu vikwazo hivyo na kusema kwamba haivikubali. Msemaji wa Rais Vladimir Putin, Dmitry Peskov, aliita hatua hiyo kuwa isiyo ya kirafiki dhidi ya Urusi na kwamba Umoja wa Ulaya unahujumu uhusiano wake na Urusi.
Jumatatu, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walikubaliana kuhusu pendekezo la pamoja lililotolewa na Ufaransa na Ujerumani la vikwazo kuhusiana na suala la kutiliwa sumu kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny.
Navalny, mpinzani mashuhuri na wazi wa Rais Putin, alisafirishwa kwenda Ujerumani siku mbili baada ya kuugua tarehe 20 Agosti mwaka huu alipokuwa katika safari ya ndege nchini Urusi. Wataalamu wa silaha za sumu wa Ujerumani walibaini kuwa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 44, alipewa sumu inayoharibu mishipa ya fahamu iliyokuwa ikitumika enzi ya Muungano wa Kisovieti.