1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Umoja wa Ulaya una sababu nyingi za kujihusisha barani Afrika"

Maja Dreyer22 Machi 2006

Masuala mawili ya kimataifa yanaangaliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo. Kwanza ni hatua ya kijeshi ya Umoja wa Ulaya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wakati wa uchaguzi mkuu. Na pili siku ya kimataifa ya maji.

Tunaanza na gazeti la “Magdeburger Volkszeitung” ambalo lina maoni yafuatayo juu ya hatua ya kupelekwa jeshi la Umoja wa Ulaya katika Kongo:

“Wakati uwezo wa hatua hiyo ya kijeshi kutokea unakua mkubwa zaidi, idadi ya wale wanaokosoa wanasiasa wa serikali yetu inazidi kuongezeka. Wanataka kujua: Kwa nini mnahatarisha maisha ya wanajeshi wetu? Suali hilo ni sawa. Lakini kosa limefanywa katika Umoja wa Mataifa mjini New York. Katika kuomba Umoja wa Ulaya kuwasaidia wanajeshi wa MONUC nchini Kongo, Umoja wa Mataifa uliangalia hasa maslahi yake binafsi.”

Na mhariri wa “Ostsee-Zeitung” la mjini Rostock anaandika:
“Licha ya hatari zote, kuna sababu muhimu kwa Umoja wa Ulaya kujihusisha katika bara la Afrika ambalo ulianzisha nalo ushirikiano wa kimkakati mwaka 2005. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo haina nguvu sana. Viongozi wa makundi ya kivita madogo madogo wana mamlaka mkubwa. Inabidi kuzuia mauaji ya kimbari yanayoweza kutokea kama nchini Rwanda au, sasa hivi tu, katika eneo la Darfur. Na juu ya hayo, Umoja wa Ulaya uligharamia uchaguzi huo kwa kutoa Dola za Kimarekani millioni 285 – fedha hizi zisilipwe bila faida lakini zihakikishe njia ya amani na uthabiti.”

Na kwa jambo la pili. Kama mlivyosikia katika matangazo yetu, leo ni siku ya kimataifa ya maji. Kuhusu siku hii, gazeti la “Nordbayerischer Kurier” limeandika:
“Suala la maji lina hatari kubwa mno, hatuwezi kuliacha kwa wanasiasa. Wakati wanasiasa fulani wanatayarisha hotuba zao ambazo wanazitoa leo hii, wengine labda tayari wanafikiria mkakati wa kudhibiti rasilimali za maji kwa njia ya kivita. Suluhisho jingine ni kuwa kila mmojawenu aanze leo na sasa hivi kupunguza matumizi yake wa maji!”

Na mwishowe ni gazeti la “Mainzer Allgemeine Zeitung” linaloandika:
“Yule ambaye anajua maji tu kuwa ni kitu cha kawaida, anayelalamika mvua na theluji ni nyingi mno, yeye bila shaka anaishi katika sehemu ya dunia hii iliyobahatika. Yule lakini ambaye hana maji, anayapigania kama katika Mashariki ya Kati au anakimbia pale ambapo bado maji yanapatikana kama barani Afrika. Ikiwa tunataka kuendelea kuishi katika sehemu iliyobahatika bila ya kuwazuia kwa kutumia nguvu wale ambao hawana maji kuja hapa, lazima tunaanza kuwasaidia sasa hivi. Kutoa pole au kusikitika tu hakutoshi. Inabidi sisi sote tupunguze matumizi ya maji na tugawe maji – na siyo kwenye siku hii ya maji.”

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW