Umoja wa Ulaya unapanga kusaidia juhudi za amani za umoja wa Afrika huko Darfour
18 Mei 2005Jumuia ya kujihami ya magharibi NATO na Umoja wa ulaya,zimeelezea utayarifu wa kusaidia juhudi za kulinda amani za umoja wa Afrika katika jimbo la Darfour.Hata hivyo taasisi hizo mbili za Ulaya zimeondowa uwezekano wa kutumwa wanajeshi katika jimbo hilo la kusini magharibi ya Sudan.Hayo yametokana na mazungumzo ya siku nzima mjini Brussels kati ya mwenyekiti wa kamisheni ya umoja wa Afrika Alpha Oumar Konare , katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO,Jaap de Hoop Scheffer na muakilishi wa siasa ya nje wa Umoja wa Ulaya Javier Solana..Maombi ya misaada ya Umoja wa Afrika yanahusu njia za usafiri kwa wanajeshi,mawasiliano,makaazi ya wanajeshi wa umoja wa Afrika na mafunzo. Umoja wa Ulaya umekubali kutoa misaada zaidi kuunga mkono juhudi za kulinda amani za Umoja wa Afrika katika jimbo la Darfour.Wakati huo huo shirika rasmi la habari la Sudan limesema serikali imeanza kuwalipa fidia raia wanaosumbuliwa na mzozo wa Darfour.Mzozo huo ulioripuka mwaka 2003 umegharimu maisha ya watu hadi laki tatu na milioni mbili wengine kuyapa kisogo maskani yao.