1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya utapambana na ukaidi wa Poland

Admin.WagnerD22 Oktoba 2021

Poland na Umoja wa Ulaya zimeshindwa kuafikiana katika siku ya kwanza ya mazungumzo, ambayo yalikusudiwa kujadili kupanda kwa bei ya nishati, lakini yaliishia kugubikwa na mzozo mkali juu ya utawala wa kisheria.

Polen  Sebastian Kaleta
Picha: Hubert Mathis/Zumapress/picture alliance

Katika mkutano wa kilele wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya uliofanyika Alhamisi; Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki alijibu ukosoaji wa umoja huo dhidi ya nchi yake huku akisisitiza hatokubali kushinikizwa.

Poland ilikosolewa vikali katika mkutano huo juu ya uamuzi wake wa kupinga kile kilichotajwa kuwa ni msingi wa kisheria wa Umoja wa Ulaya na Rais wa Bunge la Ulaya David Sassoli. Kiongozi huyo aliongeza kwamba haijawahi kutokea kwa sheria za umoja huo kutiliwa shaka na wanachama wake kama inavyofanya Poland.

Soma zaidi: Mvutano waibuka kati ya Umoja wa Ulaya na Poland

Lakini matamshi hayo yalizidi kuikasirisha Poland na Morawiecki, ambaye kipaombele chake ni kulinda  mamlaka ya nchi yake, akajibu kwamba baadhi ya taasisi za Ulaya zinaamua mambo bila ya kuwa na haki ya kufanya hivyo.

Umoja wa Ulaya hata hivyo ulishikilia msimamo wake na Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander de Croo ameikumbusha Poland kwamba kila mwanachama anafahamu wazi miongozo ya umoja huo.

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, UbelgijiPicha: Olivier Matthys/AP Photo/picture alliance

"Ikiwa unataka kuwa sehemu ya klabu, na ufaidike na klabu hiyo -- na faida zake ziko wazi kwa kila mtu, ikiwa ni pamoja na watu wa Poland -- basi unahitaji kuheshimu sheria zake. Huwezi kuwa mwanachama wa klabu halafu ukatarajia sheria zake zisikuhusu," amesema de Croo.

Hungary imeiunga mkono Poland

Hata hivyo kiongozi wa Poland alijibu kuwa nchi yake haitakubali kushinikizwa, lakini bila shaka iko tayari kutatua mizozo hiyo iliyojitokeza kwa njia ya mazungumzo.

Chimbuko la mzozo huo ni uamuzi wa Mahakama ya Katiba ya Poland mapema mwezi huu uliosema kwamba baadhi ya sheria za Umoja wa Ulaya haziendi sambamba na katiba ya nchi hiyo.

Soma zaidi:Poland yakosolewa kuwarejesha wakimbizi kinyume cha sheria 

Uamuzi huo unazifanya kambi hizo mbili kutofautiana juu ya masuala kadhaa ya kidemokrasia, kama vile uhuru wa mahakama, uhuru wa vyombo vya habari, haki za wanawake, wahamiaji na haki ya kuruhusu mapenzi ya jinsia moja.

Hungary iliiunga mkono Poland katika mkutano huo. Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban anataka kurudisha mamlaka kwenye serikali za mataifa wanachama, na amekemea kile anachoamini kuwa Tume ya Ulaya inajipa mamlaka ya kupindukia.

Tume ya Ulaya, kwa sasa, imeizuilia Poland kupata mikopo ya euro bilioni 36 ilizoomba kutoka kwenye mfuko wa fedha wa umoja huo, ili kuuinua uchumi wake ulioporomoka kutoka kwa janga la virusi vya corona.

Orban ameukemea uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya na kusema kwamba, Poland ni mojawapo ya nchi bora za Ulaya. Hakuna haja ya kuiwekea vikwazo vya aina yoyote, kufanya hivyo ni kitendo cha kijinga.

(AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW