1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya, Uturuki wakosoa sheria mpya Israel

20 Julai 2018

Umoja wa Ulaya umeikosoa sheria mpya ya utambulisho wa dola la Israel ukihofia itakwamisha juhudi za suluhisho la madola mawili huru ya Palestina na Israel, huku Uturuki ikiita sheria hiyo kuwa ni matokeo ya ubaguzi.

Jerusalem Altstadt Israelische Fahnen
Picha: picture-alliance/NurPhoto/A. Widak

Hapo jana (Alhamis 19 Julai), bunge la Israel, Knesset, liliipitisha sheria hiyo kwa kura 62 dhidi ya 55 zilizoipinga, huku wabunge wawili wakijizuwia kupiga kura zao, mmoja wao akiwa kutoka chama cha Likud kinachoongozwa sasa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. 

Benny Begin, mtoto wa kiume wa waziri mkuu wa zamani wa Israel na mwanzilishi wa Likud, Menachim Begin, alisema kuwa kwa kuja na sheria hiyo, chama chake kimejiondosha kwenye misingi ya haki za binaadamu ambayo ilikipigania.

Ukosoaji dhidi ya sheria hiyo mpya, ambayo inatamka kuwa: "Israel ni nchi ya kihistoria kwa Mayahudi na wana haki ya kipekee ya kuwa na taifa lao kwenye ardhi hii," ulitoka pia kwa Umoja wa Ulaya, mmoja wa washirika wakuu wa dola la Israel.

Kwenye taarifa yake, msemaji wa mkuu wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, alisema sheria hiyo inakinzana na suluhisho la kudumu la madola mawili huru ya Israel na Palestina. 

"Tuna wasiwasi, na tumeuweka wazi wasiwasi wetu huu na tutaendelea kuzungumza na uongozi wa Israel kwenye muktadha huu. Tumekuwa wazi sana linapokuja suala la suluhisho la madola matatu. Tunaamini ndio njia pekee ya kupita na hatua yoyote ambayo itatatiza au kuzuia suluhisho hili kutekelezeka lazima iepukwe." Ilisema taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya.

Uturuki: "Sheria ya kibaguzi"

Wabunge wa Kiarabu kwenye bunge la Israel, Knesset, wakiuchana mswada wa sheria ya utambulisho wa utaifa wa Israel siku ya Alhamis tarehe 19 Julai 2018, mara baada ya kupitishwa kwa kura 62 dhidi ya 55.Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/O. Fitoussi

Uturuki, ambayo kwa miaka mingi iliwahi kuwa mshirika wa Israel, iliikosoa vikali pia sheria hiyo. Taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki ilisema kwenye taarifa yake kwamba kuitambua haki ya utaifa wa Israel kuwa ni kwa Mayahudi pekee ni matokeo ya akili ya kale na kiyabaguzi iliyokwishapitwa na wakati.

Msemaji wa Rais Tayyip Erdogan aliitaka jumuiya ya kimataifa kuchukuwa hatua dhidi ya kile alichokiita "dhuluma inayotendeka mbele ya macho ya ulimwengu."

Msemaji huyo, Ibrahim Kalin, "hatua ya kibaguzi inayolingana na kuwafuta kabisa Wapalestina kutoka kwenye ardhi yao kimabavu na kisheria."

Sheria hiyo mpya inakifanya Kiabrenia kuwa lugha pekee rasmi na ya taifa na kukiondosha Kiarabu kutoka kwenye nafasi yake ya kuwa pia lugha rasmi. Badala yake, Kiarabu kimewekwa kwenye "nafasi maalum" ambayo, hata hivyo, inaiwezesha kuendelea kutumika kwenye taasisi za Israel. 

Vyama vya upinzani waliipinga vikali sheria hiyo bungeni. Mkuu wa chama chenye Waarabu wengi, Arab Joint List, Ayman Odeh, aliita sheria hiyo kuwa ni kifo kwa demokrasia. Wabunge wengine waliuchanachana mswaada wa sheria hiyo mbele ya spika wa bunge, Knesset, baada ya kupitishwa. 

Israel ina raia milioni 1.8 wenye asili ya Kiarabu, ambao wanaunda asilimia 20 ya wakaazi wote milioni 9 wa taifa hilo dogo la Mashariki ya Kati. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW