Umoja wa Ulaya waahirisha uteuzi wa nyadhifa za ngazi za juu
21 Juni 2019Viongozi hao wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kukutana tena Juni 30 kufikia makubaliano juu ya nani anaefaa kurithi nyadhifa tofauti za ngazi za juu, ikiwa ni pamoja na rais wa Halmashauri Kuu, baada ya kushindwa kukubaliana katika mazungumzo yaliyoendelea hadi Ijumaa alfajiri.
Viongozi wa nchi wanachama 28 wa umoja huo, walikutana mjini Brussels, Ubelgiji, kwa mazungumzo ya faragha kuhusu nani wa kuungoza Umoja wa Ulaya, huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiupinga uteuzi wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
"Baada ya mashauriano ya leo, rais wa Baraza la Ulaya ameeleza kwa uwazi kabisa kwamba hakujapatikana idadi kubwa ya uungwaji mkono kwa wakombea wote waliopendekezwa na vyama vya kisiasa. Bilashaka tunapaswa kukabiliana na hali hii," amesema Merkel akwia akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano huo.
Aidha viongozi hao wa nchi za Umoja wa Ulaya wanatarajiwa Ijumaa kuidhinisha mageuzi ya kuimarisha uchumi wa kanda inayotumia sarafu ya euro ili iweze kukabiliana na mishtuko ya kiuchumi katika siku za mbele huku wakizihimiza nchi wanachama kujikita zaidi katika hatua za maendeleo.
Idhinisho la bajeti na mchakato wa Brexit
Katika siku ya pili ya mkutano wao wa kilele ambao umetawaliwa na mkwamo wa suala la uteuzi wa nyadhifa kadhaa za ngazi za juu, viongozi hao wanatarajiwa kutia saini hatua zilizochukuliwa wiki iliyopita na mawaziri wa fedha wa mataifa yanayotumia sarafu ya euro za kuendeleza mapendekezo kadhaa ya kiuchumi. Mojawapo ya masuala yanayozozaniwa ni bajeti ya kanda hiyo inayotumia sarafu ya euro.
Mwanzoni Ufaransa ilipendekeza mfuko wa mabilioni ya euro mbali na bajeti ya Umoja wa Ulaya ambao utatumika kuimarisha uwekezaji na kufanya mageuzi ya miundo pamoja na kupunguza tofauti za kiuchumi katika mataifa ya kanda hiyo. Pendekezo hilo lilipingwa na bajeti hiyo iliyopendekezwa na Ufaransa kupunguzwa na kuamuliwa kwamba itatolewa ndani ya bajeti jumla ya Umoja wa Ulaya.
Kuhusu suala la mchakato wa Brexit, viongozi hao wamesema makubaliano yaliyofikiwa kuhusu Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya hayatofanyiwa marekebisho bila ya kujali nani atakuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.
Chanzo: (dpa,ap,rtre)