1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yaanza kuweka hifadhi ya dawa za kuzuia athari za mionzi

6 Aprili 2022

Wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutokea shambulizi la silaha za Nyuklia waongezeka Ulaya

Iod Strahlungsvorsorge Medizin Notfall 15.03.2011
Picha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Ulaya umeanza kujiandaa kuweka hifadhi ya dharura ya dawa pamoja na vifaa vya kukabiliana na athari za mionzi inayotokana na silaha za sumu.

Umoja huo leo Jumatano umefahamisha kwamba unajenga hifadhi ya dharura ya dawa na vifaa kwa Euro milioni 540. Ni hatua inayochukuliwa kufuatia wasiwasi unaoongezeka kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine.

Halmashauri ya Umoja huo ambacho ni chombo kikuu cha maamuzi katika taasisi hiyo imesema dawa, vifaa, chanjo pamoja na zana nyingine za tiba zitajumuishwa kwenye hifadhi hiyo ili kujiweka tayari kutibu wagonjwa watakaoathirika kwa sumu, silaha za kibayolojia, mionzi na nyuklia.

Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Umoja huo umebaini kwamba umeanza kununua vidonge vya kumeza vya madini ya potasium Iodide ambavyo vinaweza kutumika kumlinda mtu dhidi ya kupata athari mbaya za mionzi. Tayari vidonge milioni 3 vimeshapelekwa Ukraine kwa usaidizi wa Ufaransa na Uhispania nchi wanachama wa Umoja huo.

Janez Lenarcic ambaye ni kamishna wa kitengo cha usimamizi wa migogoro katika Umoja wa Ulaya amesema wamechukua hatua thabiti kuongeza utayarifu wa jumuiya hiyo. Tangazo la Umoja wa Ulaya limekuja wakati ikiwepo hofu inayoongezeka kuhusiana na uwezekano wa Urusi kutumia silaha za Nyuklia au za sumu kuishambulia Ukraine, nchi jirani na mshirika wa nchi za Magharibi.

Picha: Celestino Arce/NurPhoto/picture alliance

Lakini pia vita hivyo vya Ukraine vimeongeza wasiwasi kwa upande mwingine kuhusu usalama wa vinu vya Nuklia ikiwemo kile cha Chernobyl na Zaporizhia ambacho ni kinu kikubwa kabisa cha Nyuklia barani Ulaya.

Na kama haitoshi Urusi ilishakiweka kwenye hali ya tahadhari kubwa kikosi chake cha silaha za Nyuklia wakati ikitowa onyo kwa nchi za Magharibi kujiepusha kuingilia kijeshi vita hivyo kuisaidia Ukraine.