1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wachukua hatua kukabiliana na bei ya nishati

30 Septemba 2022

Makampuni ya usambazaji wa umeme katika Umoja wa Ulaya na yanayopata faida kupita kiasi yatakabiliwa na ushuru wa ziada. Hii ni kulingana na makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa Mawaziri wa nishati wa EU.

EU-Ungarn | Sitz der EU-Kommission in Brüssel
Picha: Yves Herman/REUTERS

Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Viwanda na biashara wa Jamhuri ya Czech Jozef Sikela baada ya mkutano huo wa dharura mjini Brussels nchini Ubelgiji. Sikela amesema tunaishi katika nyakati za kipekee na inapaswa kuchukua hatua haraka, zilizoratibiwa kwa uthabiti dhidi ya Urusi.

"Tuko kwenye vita vya nishati na Urusi. Majira ya baridi yanakaribia na tunahitaji kuchukua hatua sasa, kama nilivyosema. Na sasa inamaanisha leo, au labda kesho. Sio wiki na wala sio mwezi ujao. Natarajia kuwa Tume itakuja na hatua za ziada haraka iwezekanavyo, hasa kuhusu jinsi ya kupunguza bei ya gesi na jinsi ya kutoa ahueni ya haraka kwa viwanda."

Mapato na faida kulengwa

Sarafu ya Euro.Picha: Joachim Hahne/johapress/picture alliance

Ushuru huo unalenga mapato ya ziada na faida kutoka kwa makampuni ya nishati ambayo yamekuwa yakitajirika kutokana na kupanda kwa bei za nishati tangu kuanza kwa Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Pesa zitakazokusanywa na nchi wanachama zitaelekezwa kwenye kaya na makampuni ambayo yamekuwa yakikabiliwa na matatizo makubwa ya ankara za nishati.

Mtikisiko huu wa bei umesababishwa na kwamba bei ya nishati hutokana na gharama ya gesi, na ambayo imeongezeka tangu pale Urusi ilipositisha ugavi wa nishati hiyo kuelekea barani Ulaya.

Soma zaidi: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz yuko Saudi Arabia kusaka nishati kwenye nchi za Ghuba

Lakini hali hiyo ilisukuma makampuni kuzalisha umeme kwa kutumia rasilimali mbadla na za bei nafuu kama vile nyuklia huku kaya na makampuni ya biashara zikiwa katika hofu juu ya kupanda kwa bei ya nishati.

Hatua mbadala

Gharama za nishati zimepelekea kaya kuwa na hofu kuelekea msimu wa baridi Picha: DW

Mawaziri hao wa nishati wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuwepo kwa kikomo cha kiwango cha mapato hadi Juni 30 na kuamua pia kuhusu ushuru mwengine unaoitwa "mchango wa mshikamano" unaolenga faida ya ziada ya makampuni ya mafuta ambayo faida zao zimeongezeka kwa angalau asilimia 20 katika mwaka huu wa fedha ikilinganishwa na wastani wa kila mwaka.

Jumla ya hatua hizo mbili za dharura zinaweza kuzalisha hadi dola bilioni 140 zitakazotolewa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ili kufadhili hatua za usaidizi kwa watumiaji.

Soma zaidi: Viongozi walaumu hujuma kwa uvujaji wa Nord Stream 1 na 2

Kulingana na ofisi ya takwimu ya Eurostat, Bei za nishati katika Umoja wa Ulaya ziliongezeka kwa asilimia 40.8 mwezi Septemba ikilinganishwa na mwaka jana. Urusi ilipunguza kwa nguvu usambazaji wake wa gesi kwa umoja huo kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine, na kupelekea nchi za Umoja huo kununua gesi mahali pengine na kwa bei ghali zaidi.