Umoja wa Ulaya wafikia makubaliano na Uturuki
18 Machi 2016Waziri Mkuu wa Finland Juha Sipila ameandika katika mtandao wake wa Twitter kwamba makubaliano hayo na Uturuki yamefikiwa wakati viongozi wa nchi wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya walipokutana kujadili makubaliano hayo.
Afisa mwengine wa Umoja wa Ulaya aliyekataa kutajwa jina amethibitisha kufikiwa kwa makubalino hayo na kimsigi sasa inasubiriwa mazungumzo ya mwisho na waziri mkuu wa Uturuki.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Uturuki leo walikuwa katika mazungumzo magumu wakati Umoja wa Ulaya ikitaka kuwarudisha Uturuki maelfu ya wahamiaji na kupunguza shinikizo la hali ya dharura ya kibinaadamu ambalo linazidi kuugawa umoja huo.
Msimamo mgumu wa Uturuki
Akionyesha msimamo mgumu na mapema Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema wasi wasi mkuu wa serikali yake ni hatima ya takriban wakimbizi milioni 3 wa Syria walioko katika ardhi yake.Wakati huo huo waziri mkuu huyo anatarajia Umoja wa Ulaya iridhie hatua zisizo kifani za kuisogeza karibu zaidi na Umoja wa Ulaya nchi hiyo jirani.
Davutoglu amesema "Kwetu sisi,kwa Uturuki suala wakimbizi sio suala la kupatana bali ni suala la maadili ni suala zima la kibinaadamu halikadhalika ni suala la maadili la Ulaya.Uturuki imepokea wakimbizi milioni 2.7 bila ya msaada wa maana kutoka popote pale."
Davutoglu amesema anataraji mbali ya kuwasaidia wakimbizi makubaliano hayo pia yataimarisha uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Uturuki.
Kupunguzia mzigo Ugiriki
Wakati wahamiaji milioni moja wakiwa wamewasili barani Ulaya katika kipindi cha mwaka mmoja viongozi wa Umoja wa Ulaya wako mbioni kutaka kufikiwa makubaliano na Uturuki na kusuluhisha mgawanyiko mkubwa miongoni mwa nchi wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya wakati huo huo ikipunguza shinikizo kwa Ugiriki ambayo imebeba mzigo mkubwa wa kuwasili kwa wahamiaji wapya.
Mazingira ya wahamiaji nchini Ugiriki na katika kambi ya Idomeni yametajwa kuwa yasio ya kuvumulika na serikali hapo jana.Waziri wa mambo ya ndani wa Ugiriki Panagiotis Kouroumplis wakati wa ziara katika kambi hiyo ameulinganisha mji huo wa mahema sawa na kambi ya mateso na kulaumu kuteseka kwa wahamiaji kumetokana na sera za kufunga mipaka za baadhi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya.
Zaidi wahamiaji 46,000 wamenasa nchini Ugiriki baada ya Austria na nchi mbali mbali za Balkan kuzuwiya kuruhusu wakimbizi walioingia Ugiriki kutoka Uturuki kuendelea na safari kuelekea katika nchi zenye neema barani Ulaya.
Chini ya makubaliano hayo Umoja wa Ulaya utalipia wahamiaji wapya wanaowasili Ugiriki ambao hawastahiki kupatiwa hifadhi kurudi Uturuki. Kwa kila Msyria mmoja anayerejeshwa,Umoja wa Ulaya itakubali kumpokea mkimbizi mmoja wa Syria na kufikia hadi watu 72,000 watakaogawanywa katika mataifa ya Ulaya.
Mbali na kuregeza masharti ya visa Umoja wa Ulaya pia utaipatia Uturuki msaada wa hadi euro bilioni sita pamoja na kuharakisha mazungumzo ya Uturuki kujiunga na umoja huo.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP
Mhariri :Yusuf Saumu