1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya watofautiana juu ya Urusi

24 Juni 2021

Nchi za Umoja wa Ulaya ambazo ni jirani wa Urusi haziungi mkono kukaa kwenye meza ya mazungumzo na Urusi wakati Ujerumani na Ufaransa zikipigia upatu kukaa na nchi hiyo

Deutschland Treffen Merkel und Macron in Berlin
Picha: Axel Schmidt/dpa/Reuters/picture alliance

Viongozi wa nchi na serikali za Umoja wa Ulaya wanakutana kwenye mkutano wa kilele jioni hii huku suala la Urusi likiwa agenda inayozungumziwa kwa kiwango kikubwa. Baadhi ya viongozi wa umoja huo wanaunga mkono hatua ya kukaa chini kwenye meza ya mazungumzo na Urusi na wengine wakiipinga kabisa hatua hiyo.

Mgawanyiko miongoni mwa viongozi wa Umoja wa Ulaya  kuhusu namna ya kuishughulikia Urusi  ndio hasa unaozungumziwa hapa, ambapo inatarajiwa kikao hicho cha leo kitashuhudia kauli na misimamo ya kila upande kuhusu suala hilo. Lakini pia ni kikao kitakalizungumzia suala la uhusiano uliopo na Uturuki.

Picha: Francois/Walschaerts/AFP/Getty Images

Mkutano huu ni wa siku mbili na kabla ya kuanza kansela wa Ujerumani Angela Merkel alitowa hotuba mbele ya bunge la nchi yake,bundestag na miongoni mwa aliyoyasema ni kuwasisitiza viongozi wa Umoja wa Ulaya kutafuta msimamo wa pamoja kuelekea Urusi. Na hata alipowasili Brussels alirudia tena kusema kwamba mazungumzo ndio njia pekee ya kutatua matatizo.

    " Kama tulivyoona kwa rais wa Marekani, migogoro  inaweza kutatuliwa kwa ubora zaidi kupitia mazungumzo.Kwahivyo tutayajadili mengi.Asanteni nasubiria mazungumzo.''

Kansela Merkel anasema kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa  kutafuta mfumo utakaouwezesha  kujibu uchokozi wa Urusi kwa pamoja na kwa mshikamano na ni kwa njia hiyo tu ndipo Umoja huo utakapoweza kukabiliana na mashambulizi mbali mbali ya Urusi.

Picha: Denis Balibouse/REUTERS/AP/picture alliance

Lakini inaonesha Umoja wa Ulaya haukubaliani kwa sauti moja na mtazamo huo wa Merkel unaopigiwa debe pia na Ufaransa. Ujerumani na Ufaransa zinapendekeza ufanyike mkutano wa moja kwa moja na Urusi lakini nchi nyingi za Umoja huo haziafiki wazo hilo wakati nyingine zina mashaka makubwa. Kwa mfano Uholanzi waziri mkuu wake Mark Rutte anasema ingawa hapingi mkutano wa moja kwa moja na Urusi lakini yeye hawezi kushiriki mkutano wa aina hiyo. Huku rais wa Lithuania Gitanas Nauseda akisema.

"Ikiwa hakuna mabadiliko yoyote mazuri katika tabia ya Urusi na tukajiingiza kwenye mazungumzo itapeleka ujumbe wa mashaka makubwa na kutoa dalili mbaya kwa washirika wetu kwa mfano wa nchi za Mashariki''

 Wakati nchi zinazopakana na Urusi zikionesha mashaka ya kuisogelea Urusi,Urusi yenyewe imeliafiki wazo la kuwepo mazungumzo. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema rais Putin anaunga mkono pendekezo la kuweka mfumo wa kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Brussels na Moscow.

Picha: OLIVIER MATTHYS/AFP via Getty Images

Mkutano utajadili pia suala la Uturuki ambapo tayari kansela wa Austria Sebastian Kurz amesema kile ambacho Umoja wa Ulaya hautakiwi kukifanya ni kutoifumbia jicho Uturuki na kukubaliana na kinachofanywa na nchi hiyo ambacho kwa upande mwingine kinakosolewa kinapofanywa na mataifa mengine. Ametowa mfano kwamba Umoja wa Ulaya umeikosoa sana Belarus lakini kinachofanywa na nchi hiyo hata Uturuki kinafanyika na hali nchini humo pia ni mbaya.