Umoja wa Ulaya waghadhabishwa na shambulizi la Urusi
28 Agosti 2025
Umoja wa Ulaya umemwita balozi wa Urusi mjini Brussels Alhamisi, baada ya mashambulizi makubwa ya Urusi dhidi ya Kiev huko Ukraine ambayo yamesababisha vifo vya watu 14.
Mashambulizi hayo ya droni pia yaliharibu jengo la ujumbe wa kidiplomasia wa umoja huo.
Mkuu wa Halmshauri Kuu ya umoja huo Ursula von der Leyen ameyataja mashambulizi hayo kuwa uthibitisho kwamba Urusi haipo tayari kusitisha vita na ameahidi kuongeza shinikizo zaidi dhidi ya Moscow.
"Nimeghadhabishwa na shambulizi dhidi ya Kiev ambalo pia limepiga ofisi zetu za Umoja wa Ulaya. Hili ndilo shambulizi baya zaidi la droni na makombora mjini Kiev tangu Julai. Na unavyoona kwenye picha lilikuwa pia shambulizi dhidi ya ujumbe wetu," amesema von der Leyen.
Von der Leyen ametangaza kuandaa awamu nyingine mpya ya vikwazo dhidi ya Urusi, mnamo wakati maafisa wa Marekani na Ukraine kukutana Ijumaa.
Viongozi mbalimbali wameilaani Urusi kwa shambulizi hilo akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na wakuu wengine ambao ni wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.