151112 EU-Außenminister Mali Syrien
16 Novemba 2012Kundi la nchi tano za Umoja wa Ulaya ambazo ni Ujerumani,Ufaransa Poland,Itali na Spain zimekuja pamoja kujaribu kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Mali ikiwa ni pamoja na kuzishawishi nchi nyingine za umoja huo wenye wanachama 27 kusaidia katika kuwapa mafunzo wanajeshi wa Mali kupambana na waasi na hatimae kulikomboa eneo la Kaskazini.
Mawaziri wa ulinzi na mambo ya nje kutoka nchi hizo tano waliokutana hapo jana mjini Paris nchini Ufaransa walijadiliana juu ya masuala mbali mbali ikiwemo mgogoro wa Syria lakini zaidi walijikita katika suala la Mali wakisema kwamba kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayoukabili umoja wa Ulaya itakuwa ni jambo la busara zaidi kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja hasa baada ya Marekani kutoa kauli yake kwamba Umoja huo unabidi sasa kushughulikia mizozo iliyoko mlangoni kwake,katika eneo la bahari ya Meditterenia na Afrika.
Ni kutokana na kauli hiyo nchi tano ambazo zimekuwa tangu mwanzo zikijishughulisha na kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa mali zinataka umoja wa Ulaya kwa jumla kujitolea kuchangia katika utoaji wa mafunzo kwa wanajeshi wa mali.Kauli ya Mawaziri wa Ulinzi na wa mambo ya nje wa nchi hizo imeonya kwamba mtandao wa kigaidi Kaskazini mwa nchi hiyo unapata nguvu na kuna wasiwasi kwamba huenda ukadhibiti pia biashara ya madawa ya kulevya kuingia ulaya na kwa maana hiyo mgogoro wa Mali sio suala la Mali tu bali ni tatizo la Ulaya kwa jumla.Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesisitiza wakati umefika kwa Umoja huo kushirikiana kuumaliza mgogoro huu.
Itakumbukwa kwamba mwezi Uliopita mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walisema Umoja huo utakuwa tayari kusadia katika kuijenga upya nchi hiyo na pia kukipa mafunzo vikosi vya ulinzi vya Mali.Catherine Ashton mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja huo alitwikwa jukumu la kuandaa mipango wa jeshi litakalohusika na mafunzo hayo kufikia Novemba 19.Ujerumani ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizokubali kutoa wanajeshi wake kwa ajili ya kushiriki inasisitiza kwamba upo umuhimu wa mazungumzo ya kutafuta suluhu kuendelea.
Ujerumani,Ufaransa,Poland,Itali na Uhispania kwa hivyo zinatarajiwa kutoa mapendekezo yake mbele ya wanachama wote wa Umoja huo mjini Brussels.
Mwandishi:Seibert Evi zpr/Saumu Mwasimba-(DPA)
Mhariri:Mohammed AbdulRahman.