1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wahofia ukandamizaji, Belarus

7 Septemba 2020

Msemaji wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Peter Stano amesema umoja huo una taarifa kuhusu madai ya kutekwa kwa mwanaharakati huyo pamoja na wanaharakati wengine wa kisiasa.

Kiongozi wa maandamano Belarus Maria Kolesnikova
Kiongozi wa maandamano Belarus Maria KolesnikovaPicha: picture-alliance/dpa/S. Bobylev

Umoja wa Ulaya umesema una wasiwasi kuhusiana na ripoti za hivi karibuni za kukamatwa wanaharakati wa kisiasa nchini Belarus. Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi huo kufuatia ripoti za katekwa kwa aliyekuwa kiongozi wa maandamano Maria Kolesnikova.

Msemaji wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Peter Stano amesema umoja huo una taarifa kuhusu madai ya kutekwa kwa mwanaharakati huyo pamoja na wanaharakati wengine wa kisiasa. Amesema, kimsingi kile wanachokishuhudia ni mwendelezo wa ukandamizaji unaofanywa na mamlaka dhidi ya raia na kuelezea wasiwasi kuhusu kuendelea kwa hatua hizo zinazochukuliwa kwa mirengo ya kisiasa. Akasema, hilo halikubaliki.

Ripoti za mapema hii leo zilisema mwanaharakati huyo Maria Kolesnikova ametekwa na watu wasiojulikana katikati ya mji mkuu Minsk na kumpakiza kwenye gari na kuondoka naye, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la Tut.By la Belarus.

Waandamanaji Belarus wanaupinga utawala wa Rais Alexander LukashenkoPicha: picture-alliance/AP Photo/TUT.by

Mpinzani mkubwa wa rais Alexander Lukanshenko, Sviatlana Tsikhanoviskaya amelitaja tukio hilo la kutekwa kama jaribio la mamlaka la kudhoofisha uratibu wa baraza la upinzani na kuwatisha wajumbe wake.

Tukio hilo la kutekwa iwapo litathibitishwa linakuja wakati mamlaka za Belarus zikionekana kuimarisha juhudi zake za kujaribu kuyavunja maandamano yanayozidi kupata nguvu.

Katika hatua nyingine, Umoja wa Ulaya unalenga kuwawekea vikwazo vya kiuchumi maafisa 31 wa Belarus ikiwa ni pamoja na waziri wa mambo ya ndani ifikapo katikati ya mwezi huu.

Wanadiplomasia watatu wa Umoja wa Ulaza wamesema hatua hiyo inafuatia uchaguzi wa Agosti 9, ambao mataifa ya magharibi yanasema ulivurugwa.

Rais wa Belarus Alexander LukashenkoPicha: picture-alliance/AP Images/N. Petrov

Mmoja wa wanadiplomasia hao amesema, awali walikubaliana majina 14, lakini mataifa mengi yalihisi kwamba hayakutosha na baadaye kukubaliana majina mengine 17 ya maafisa waliohusika na uchaguzi huo, machafuko na hatua kali zinazochukuliwa nchini humo.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja huo, waliunga mkono hatua hiyo ya vikwazo ambavyo ni pamoja na kuwazuia kusafiri kuingia mataifa ya umoja huo na kuzuia mali zao wakati wa mkutano mjini Berlin mwishoni mwa mwezi uliopita lakini hawakuwa wamekubaliana kuhusu walengwa. Kilichosalia sasa ni muda muafaka wa utekelezaji wake.

Lukashenko alidai kushinda kwa asilimia 80 kwenye uchaguzi wa urais, lakini mpinzani wake Tikanoviskaya anasema uchaguzi huo ulivurugwa na kutoa mwito wa mapinduzi ya amani kuhitimisha utawala wa Lukashenko.